MAGARI yameanza kupita daraja la Kiyegeya wilayani Kilosa mkoani Morogoro, ambalo lilikatika Jumatatu wiki hii, magari hayo yalianza kupita tangu juzi usiku na yanapita kwa zamu.
Hata hivyo, imeibuka foleni ya magari hasa malori, kutokana na upitishaji wa magari machache kwa kila upande wa daraja hilo. Foleni hiyo ya malori imeonekana pande zote mbili.
Kwa upande wa kutoka Morogoro-Dodoma, foleni imefika umbali wa kilometa 15 hadi 20 kutoka eneo la Kwambe, lilipokatika daraja hilo. Kwa upande wa kutoka Dodoma– Morogoro, foleni hiyo imeenda hadi Gairo, kiasi cha kilometa 30 hadi lilipo daraja hilo Jeshi la Polisi limeonekana kusimamia kikamilifu zoezi la kuruhusu magari hayo kupita kwa zamu.
Nao wahandisi na mafundi kutoka Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) na Kampuni ya Yapi Markezi (inayojenga Reli ya Kisasa –SGR), wanaendelea kutengeneza njia ya mchepuko, itakayotumiwa na magari wakati daraja likiimarishwa na kutengenezwa.
Akizungumzia katika eneo lilipokatika daraja hilo, jana, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani cha jeshi hilo, Fotunatus Muslimu alisema wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupitisha kwa utaratibu magari madogo na mabasi, yaliyokwama muda mrefu katika eneo hilo. Muslimu alisema kipaumbele kikubwa ni mabasi ya abiria, magari yaliyobeba wagonjwa na yale yanayosafirisha miili.
Aliwataka madereva wanaotumia barabara hiyo ya Morogoro-Dodoma, kuendelea kutumia njia mbadala. Wale wanaotoka Dodoma wapitie Babati mkoani Manyara, Arusha hadi Dar es Salaam.
Wale wanaotoa Dar es Salaam kwenda Dodoma, watumie barabara ya Morogoro-Iringa-Dodoma. Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema barabara ya Morogoro-Dodoma ilitengenezwa miaka 40 iliyopita, hivyo umri wake ni mkubwa, na ndio maana wamekuwa wakiifanyia ukarabati wa mara kwa mara. Mfugale alisema kukatika kwa daraja la Kiyegeya ni jambo la kawaida kiutaalamu.
Alisema makalavati yanayowekwa kwenye madaraja, uhai wake wa kuishi huwa sio zaidi ya miaka 25, wakati barabara hiyo, lilipokatika daraja hilo, ina zaidi ya miaka 40 na tayari ni chakavu.
Alibainisha kuwa serikali iko kwenye mchakato wa kujenga upya barabara hiyo ya Morogoro-Dodoma na madaraja yake. Hakutaja gharama za ujenzi huo. Pia, Mfugale alizungumzia mikakati yao ya kujenga barabara ya mchepuko na kukamilisha haraka daraja hilo lililokatika ili lipitishe magari. Alisema ndani ya wiki moja ujenzi huo utakuwa umekamilika.
Chanzo: Tovuti ya HabariLeo
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.