Maisha ya watu yanafupishwa na magonjwa yasiyoambukiza kutokana na maradhi ya Moyo, Kisukari, Saratani, Magonjwa ya njia ya hewa, Siko Seli, ajali, magonjwa ya figo, akili, dawa za kulevya na magonjwa sugu ya meno na macho.
Hayo yamesemwa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi (pichani) ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya wakati akifungua kongamano la pili la kitaifa la kisayansi la magonjwa yasiyoambukiza linalofanyika kwenye ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.
Prof. Makubi amesema kuwa magonjwa hayo yamesababisha hasara kubwa kwa taifa kwa maana ya kuondoa nguvu kazi na kurudisha nyuma maendeleo ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla na hivyo kusababisha utegemezi sugu kwa familia na pia kuongeza mzigo mkubwa kwenye mfumo wa afya kwa kuwa ni magonjwa ya muda mrefu na yanatumia rasilimali nyingi.
Akielezea hali ya magonjwa hayo Mganga Mkuu huyo alitaja takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa magonjwa hayo yamesababisha asilimia 33 ya vifo vyote nchini kwa mwaka 2017, ambapo jumla ya vifo 134,600 viliripotiwa na kuhusishwa na magonjwa yasiyoambukiza.
“Vifo hivi vimetokana zaidi na magonjwa ya moyo na shinikizo la damu kwa asilimia 13, Kisukari 2%, Saratani 7% na ajali 11%, hali hii kwa ujumla haikubaliki na inatufanya tujumuike katika kujitathimini na kupanga mikakati ya pamoja ili kukabiliana na changamoto hii”. Alisisitiza Prof. Makubi.
Aidha, amesema takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza yanachangia zaidi ya vifo milioni 41 ambayo ni sawa na asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 vilivyotokea mwaka 2016.
Aliongeza kuwa Magonjwa yasiyoambukiza yanachangia zaidi ya robo tatu (75%) ya vifo ambavyo kama ugonjwa ungetambulika mapema vingeweza kuepukika na huku mataifa ya uchumi wa kati na chini kama Tanzania yanaonekana kuathirika zaidi.
Hata hivyo Prof. Makubi aliwapongeza wanasayansi ambao wamewasilisha maandiko yao katika kongamano hilo ili kutoa ushahidi wa kisayansi wa ukubwa wa changamoto zilizopo katika kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza na ushauri wa namna ya kuzitatua.
Pichani chini ni baadhi ya washiriki wa kongamano la pili la kitaifa la kisayansi la magonjwa yasiyoambukiza linalofanyika kwenye ukumbi wa JNICC jijini Dar es Salaam.
Chanzo: Wizara ya Afya
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.