MAGONJWA yasiyoambukiza (NCDs) yanachangia takribani 33% ya vifo vyote nchini huku kwa takwimu za Shirika la Afya duniani (WHO) kwa mwaka 2020 zinaonesha kuwa magonjwa hayo yalichangia zaidi ya vifo milioni 41 sawa na 71% ya vifo vyote Duniani .
Hayo yalielezwa leo na Waziri wa Afya kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Ally Mazrui wakati wa Uzinduzi wa Utafiti wa Kitaifa wa Viashiria vya Magonjwa Yasiyoambukiza (STEPS SURVEY 2023) uliofanyika kwenye ukumbi wa Takwimu Jijini Dodoma.
Mhe. Mazrui alisema takwimu zinaonesha kuwa magonjwa hayo yameongezeka mara 5 hadi 9 zaidi kati ya miaka ya 80 ambapo 1% tu ya watanzania walikuwa na tatizo la kisukari na 5% walikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu wakati kwa sasa tatizo la kisukari limefikia asilimia 9 na tatizo la shinikizo la juu la damu limeongezeka na kufikia asilimia 25.
“Takwimu zinaonyesha kuwa kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya nchini kumekuwa na ongezeko kubwa sana la magonjwa hayo ambapo katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023, Magonjwa yasiyoambukiza yalisababisha wagonjwa wengi kuhudhuria vituo vya huduma za afya wakiwemo wagonjwa wa shinikizo la juu la damu wagonjwa 1,456,881 sawa na asilimia 49 ukilinganisha na asilimia 34 kipindi kama hicho mwaka 2021/2022 ,Kisukari wagonjwa 713,057 sawa na asilimia 24, magonjwa ya mfumo wa hewa wagonjwa 386,018 sawa na asilimia 13 ikilinganishwa na asilimia 10 kwa kipindi kama hicho mwaka 2021/2022.
Naye Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Afya kutoka Ofisi ya Rais -TAMISEMI Dkt. Wilson Mahera amesema matokeo ya utafiti huo yatasaidia katika sekta ya afya hususan katika ngazi ya msingi ili kuweza kupunguza changamoto za matibabu kwani wananchi wengi zaidi ya 90% wanaanzia kupata huduma za afya ngazi za msingi na pia Serikali imeweza kuboresha miundombinu ya kutolea huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Dkt. Mahera amesisitiza Mikoa, Halmashauri na vituo vya afya kuwa na mipango ya bajeti sahihi ambayo inalenga mahitaji sahihi ya magonjwa yasiyoambukiza kwani kuwa na takwimu sahihi itasaidia kuweka mipango mizuri ya kupambana na magonjwa hayo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.