Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge amewataka wawekezaji, wafanyabiashara na wananchi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha wanachangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika Jiji hili linalokua kwa kasi ili kuweza kuendana na hadhi ya Makao Makuu yenye ubora katika sekta zote.
Kauli hiyo ameitoa katika kikao cha tathmini ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa mikutano wa Halmashauri.
Dkt. Mahenge amesema wakati umefika sasa kwa wawekezaji kutambua na kuchangamkia nafasi zilizopo kwa kuitumia miradi hiyo, ambayo ina miundombinu rafiki ya kuwawezesha kufanikisha malengo yao katika utoaji huduma, pia kuwawezesha kuinua viwango vya huduma na kufanya viwe vya kimataifa ili kukidhi matakwa ya watumiaji.
“Dodoma kuna fursa nyingi, tuna miradi ya kimkakati ambayo iko katika hatua za mwishoni kumalizika ili ianze kutumika. Lipo soko, kituo cha mabasi, bustani ya mapumziko ya Chinangali, na kituo cha malori Nala, pia kuna miradi ambayo kulingana na Jiji letu kuwa Makao Makuu tumepata neema serikali itajenga uwanja wa ndege na kiwanja cha mpira vyote vyenye hadhi ya kimataifa.
“Lazima tuwe na mipango mikakati mizuri ya kuwawezesha wawekezaji wenye uthubutu wawekeze hapa, kwa sababu tuna miradi yenye viwango vya kimataifa hivyo ni lazima huduma zetu za afya, elimu, na huduma nyinginezo nazo tuziweke katika hadhi hiyo ili wageni mbalimbali wapate nafasi ya kufurahia uwepo wao ndani ya Jiji letu,” alisema Dkt. Mahenge.
Mbali na kuizungumzia miradi hiyo ya kimkakati Mkuu huyo wa Mkoa pia ametoa ushauri kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuhakikisha anaweka mipango thabiti itakayowezesha wananchi kufanya shughuli zao ikiwemo uuzaji na ununuzi wa bidhaa madukani, kuwa na miundombinu rafiki kwao na usalama wa mali zao.
“Utekelezaji wa hayo yote utatokana na mipango mizuri mtakayokuwa nayo, kwa mfano ukizunguka maeneo ya mjini kuanzia barabara 7 na kuendelea sehemu zote zilizotengwa kwa ajili ya maegesho ya wateja hivi sasa wamiliki wa maduka wamegeuza na kuweka magari yao wenyewe.
“Hali inayosababisha usumbufu kwa wateja wanapoenda na magari yao, lakini pia mnaweza kuongea na wahusika wa Shirika la Reli Tanzania ili wawapatie eneo la Jamatini mlitumie kama eneo la maegesho ambapo pia mtaingiza mapato, wateja wakilipa kwa masaa sio vibaya ili eneo la mjini libaki kuwa wazi bila msongamano wa magari” alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amemtaka Mkurugenzi kuweka usimamizi mzuri ifikapo wakati wa zoezi la ugawaji wa maeneo katika miradi ya kimkakati kwa wafanyabiashara watakaopatiwa nafasi, na zoezi liendeshwe kwa umakini, uhuru na haki ili kuepukana na madalali watakaoweza kujitokeza na kulitia doa zoezi hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge alipotembelea Jiji la Dodoma akiambatana na Katibu Tawala wa Mkoa, na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Patrobas Katambi na maafisa kutoka ofisi yake. Pichani anaonekana Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Godwin Kunambi (aliyesimama) akimukaribisha ujumbe huo.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Patrobas Katambi (katikati) akipokea makablasha yenye maelezo kuhusu miradi ya uwekezaji na uendeshaji wake kutoka kwa Mkurugenzi wa Jiji Godwin Kunambi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.