IKIWA ni Wiki ya Mazingira, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha wanaweka mikakati endelevu ya uhifadhi mazingira kwa kuhakikisha maeneo yote yanayopimwa yanapandwa miti.
Hatua hiyo imekuja kufuatia ripoti ya Mazingira nchini kuonyesha kiwango cha ukataji miti katika mkoa huo kuwa ni wastani wa hekta 3,730,000 kwa Mwaka kiasi ambacho amekitaja kuwa ni kikubwa sana kinachopelekea hali ya ukame zaidi.
Hayo yameelezwa jana Jijini hapa na Waziri Mkuu wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya mazingira duniani ambalo hufanyika kuanzia Juni 1 hadi 5, 2021 kwa lengo la kuikumbusha jamii umuhimu wa uhifadhi mazingira.
Akiongea kwenye uzinduzi huo amesema kutokana na ripoti ya mazingira kuonyesha kuwa Dodoma ni mkoa unaokabiliwa na ukame nchini, uongozi huo uhakikishe kila mwananchi anayepata kiwanja anaelimishwa kuhusu umuhimu wa kupanda miti ili kuunusuru mkoa wa Dodoma na hali ya ukame.
Amesema changamoto nyingi za mazingira zimeonekana katika Mkoa wa Dodoma hivyo kuutaja mkoa huo kuwa mwenyeji wa Maadhimisho hayo Kitaifa yanayoyarajiwa kuwafanyika Juni 5.
"Kutokana na ripoti ya mazingira kuonyesha kuwa Dodoma ni kame kwa mwaka huu Serikali imeamua kufanya Maadhimisho Kitaifa Mkoani hapa ili kuwakumbusha wakazi wake kuwa makini kwa utunzaji mazingira," alisema.
Kutokana na hayo Waziri Majaliwa alitolea mfano wa ripoti ya tatu ya hali ya mazingira nchini iliyofanyika mwaka 2019, ikionyesha Dodoma Kuwa ni miongoni mwa maeneo ya ukame na yana kasi kubwa ya ukataji wa miti.
"Ni wakati sasa wa kuendelea kubuni nishati mbadala, kiwango hicho kinaonyesha kusababishwa na mahitaji makubwa ya nishati ya kuni na mkaa, lazima tushirikiane kuhakikisha Dodoma inakuwa ya kijani,"alisisitiza.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Selemani Jafo ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa katika Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira, shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwemo maonesho ya mazingira kupitia taasisi zaidi ya 100.
"Katika maonyesho hayo wakazi wa Dodoma watapata nafasi ya kujifunza teknolojia mbalimbali za nishati mbadala ili kuondokana na uharibufu wa mazingira kwa kukata miti kwa matumizi ya nyumbani," alisema Jafo.
Pamoja na hayo aliongeza kuwa wiki hiyo pia itahusisha semina itakayowashirikisha maofisa mazingira nchini kutoka katika wizara, taasisi na mamlaka za Serikali za mitaa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.