WATANZANIA wameelezwa kuwa namna nzuri ya kumuenzi aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ni kuyaishi maono ya utumishi wake katika kufanya kazi kwa bidii.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa leo katika uwanja wa Jamhuri, jijini hapa wakati wa hafla rasmi ya kitaifa ya kuuaga mwili wa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli iliyohudhuriwa na viongozi kutoka mataifa mbalimbali na wananchi wa Jiji la Dodoma na mikoa ya jirani.
Waziri Mkuu Majaliwa amesema “namna nzuri ya kumuenzi Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ni kuishi utumishi wake uliojaa maono na mapenzi katika utumishi wake. Maono hayo ni kufanya kazi kwa bidii, kwa kuzingatia umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Na katika kipindi hiki cha maombolezo, tuzidishe upendo, umoja na mshikamano miongoni mwetu”.
Waziri Mkuu huyo amezishukuru nchi jirani na kuwaombea kuendelea vizuri katika utekelezaji wa majukumu yao. “Leo tumethibitisha upendo wenu kwetu, kuwapata Marais tisa siyo jambo dogo, kuwapata Makamu wa Rais wawili siyo jambo dogo. Jambo hili linaonesha upendo mkubwa walionao dhidi yetu” alisema Majaliwa.
Akisoma wasifu wa Hayati, Dkt. Magufuli, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa, Prof. Paramagamba Kabudi amesema kuwa kisiasa, Hayati Dkt. Magufuli aligombea ubumbe katika Jimbo la Bihalamulo mashariki mwaka 1990 na hakufanikiwa. Mwaka 1995 aligombea tena ubunge katika uchaguzi mkuu wa vyama vingi na kushinda Jimbo la Bihalamulo Mashariki. Mwaka 2000 na mwaka 2005 aligombea ubunge Jimbo la Bihalamulo Mashariki na kupita bila kupingwa. Baada ya kugawanywa jimbo hilo, mwaka 2010, aligombea ubunge jkupitia Jimbo la Chato, na kupita bila kupingwa.
Waziri kabudi amesema kuwa mwaka 2015, alikuwa miongoni mwa makada wa Chama cha Mapinduzi waliochukua fomu kuomba kupeperusha bendera ya CCM katika nafasi ya urais. Aliteuliwa na chama chake kupeperusha bendera hiyo na kushinda urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.