WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Ofisi ya Rais-TAMISEMI ihakikishe inasimamia ujenzi wa majengo ya ofisi za halmashauri ya wilaya ya Kigoma unafanyika kwenye Kata ya Mahembe kama ilivyopendekezwa katika vikao vya Baraza la Madiwani, si katika Kata ya Kamala linalopendekezwa na wataalamu.
Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Septemba 17, 2021) mara baada ya kusimamishwa na wakazi wa kata hiyo ambao wamedai maamuzi ya madiwani yamebadilishwa na kusisitiza kuwa kama sababu ni eneo kutofaa kwa ujenzi wa majengo ya ghorofa wabadilishe ramani Ili yajengwe majengo ya kawaida.
Wananchi hao ambao waliwasilisha malalamiko yao kupitia mabango walimueleza Waziri Mkuu kwamba hawaridhishwi na maamuzi ya Serikali ya kuhamishia ujenzi wa ofisi za halmashauri katika Kata ya Kamala wakati Baraza la Madiwani lilishatoa maamuzi kupitia vikao rasmi.
Akijibu malalamiko hayo Mhe. Majaliwa alisema “Katibu Tawala wewe unajua kwamba maamuzi ya ujenzi wa Halmashauri yanaamuliwa na wananchi wenyewe kupitia Baraza lao la Madiwani, na Baraza la Madiwani limekaa mara tatu, na wewe ndio msimamizi wa Halmashauri zote kwenye mkoa huu, maamuzi haya bado yatabaki kuwa maamuzi ya Halmashauri.
Kama eneo hilo sababu ni hizo za kwamba eneo ghorofa halifai, ni lazima mjenge maghorofa? umuhimu ni kujenga majengo ya kutolea huduma, ghorofa sio lazima! Ili mradi wanaMahembe wametoa ekari 20, na ni muhimu kupata eneo kubwa ili mjenge hizo ofisi zenu na nyumba mjenge hapo, nyumba nyingine mjenge hapo, muweke na viwanja vya michezo… huko (kwingine) msijenge” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa na wananchi wa kata ya Mahembe.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.