Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha kuanzia sasa vyakula kwenye migodi havitoki nje ya nchi na badala yake watumie vinavyozalishwa nchini.
Pia amekemea ukamataji holela wa wawekezaji na wadau wa madini, akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufuata sheria, kanuni na miongozo inayosimamia sekta hiyo.
Majaliwa alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akifunga semina maalum ya vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu usimamizi wa rasirimali madini iliyofanyika jijini hapa.
Alisema katika kipindi cha hivi karibuni, kumejitokeza malalamiko mengi kutoka kwa wawekezaji na wadau wa madini kuhusu kukamatwa au kubughudhiwa bila sababu za msingi.
"Natumia nafasi hii kukemea suala la ukamataji holela wa wawekezaji au wadau wa madini pasipo kufuata taratibu. Hivyo basi, tumieni sheria, kanuni na miongozo mbalimbali iliyowekwa mahsusi kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa sekta ya madini," aliagiza.
Alisema uanzishaji wa masoko ya madini ni sehemu ya mkakati mahsusi wa serikali kupunguza utoroshwaji wa madini kwa kuwa awali ilionekana kuna utoroshaji mkubwa unaofanyika kwa kisingizio cha kutafuta soko.
"Hata hivyo, kuna tatizo lingine limeanza kujitokeza la kuwakamata wadau wakiwa na madini hata kama wanapeleka sokoni," alisema.
Aliagiza kuanzia sasa wadau wote wanaopatikana na madini, wapewe utaratibu wa kuelekea sokoni kuuza badala ya kuwakamata wakiwa wanaenda sokoni.
"Ni wajibu wetu kusimamia na kudhibiti utoroshwaji wa madini na pia ni jukumu letu sisi kama vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha kuwa masoko haya pamoja na wafanyabiashara ya madini wanaofanya kazi zao kwa kufuata sheria wanalindwa na kuepuka kamata kamata zisizo na tija," aliagiza.
Alisema kuna wakati hawahitaji kutumia nguvu nyingi bali kutoa ushauri tu ili kutatua shida husika.
Kuhusu vyakula, Waziri Mkuu alisema vyombo hivyo vinapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha huduma za vyakula migodini kuanzia sasa hazitoki nje ili bidhaa zilizopo nchini zitumike.
"Unakuta mchele wanaoutumia wafanyakazi wa migodini unatoka nje, jambo ambalo halikubaliki kwa sababu mchele tunalima sisi wenyewe, hivyo naagiza suala hilo likafanyiwe mabadiliko," alisema.
Waziri wa Madini, Dotto Biteko, alitangazia 'vita' dhidi ya watu wanaouza madini feki na kuwataka waache mara moja kwa kuwa tayari wamewabaini.
"Tunaomba wanaofanya hivyo waache mara moja, tunaanza msako wa kuwatafuta watu wa aina hii," alionya.
Chanzo: www.ippmedia.com
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.