WAZIRI MKUU wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) amewaagiza Mawaziri na Makatibu Wakuu wasimamie kikamilifu awamu ya pili ya mpango wa ujenzi wa Mji wa Serikali ulipo Mtumba jijini Dodoma ili ukamilike kwa wakati.
Ametoa agizo hilo jana (Jumatano, Septemba 8, 2021) wakati akiongoza Kikao Kazi cha Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Naibu Katibu Wakuu pamoja na Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuratibu Mpango wa Serikali wa Kuhamia Dodoma katika ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi hao wahakikishe wanasimamia kikamilifu ujenzi huo ambao utatekelezwa kwa awamu mbili kwa mwaka wa fedha 2021/2022 na 2022/2023.
“Katika kufanikisha ujenzi huu ni vyema tukahamasisha sekta binafsi kufanya uzalishaji ili kuweza kuwa na uhakika wa upatikanaji wa vifaa vya ujenzi ikiwemo tofali, mchanga na kokoto.”
Waziri Mkuu amesema, baadhi ya Wizara tayari zimeanza taratibu za manunuzi na kuzitaka zile ambazo bado zihakikishe zinakamilisha utaratibu wa zabuni hadi kufikia mwishoni mwa Septemba, 2021.
“Taasisi zote zitakazo husika na ujenzi wa majengo haya, hakikisheni unakuwa ni wa viwango na wenye ubora na hakutakuwa na ucheleweshaji katika ujenzi.” alisisitiza Waziri Mkuu Majaliwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.