JUMLA ya wawakilishi wa makampuni 13 ya kibiashara kutoka nchini Austria wamefika Jijini Dodoma kwa lengo la kutafuta fursa za uwekezaji katika nyanja tofauti za kiuchumi.
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru aliupokea msafara wa wageni hao uliowasili katika uwanja wa ndege Jijini humo Disemba Mosi, 2020 saa 11:00 jioni kwa ndege ya shirika la ndege la Tanzania (ATCL) wakiwa wameambatana na maofisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi ya Tanzania.
Akizungumza uwanjani hapo mara baada ya kuupokea msafara huo, Mkurugenzi Mafuru alisema makampuni hayo yanatarajia kufanya uwekezaji mkubwa kutokana na fursa zilizopo jijini humo.
Alisema msafara wa makampuni hayo umeratibiwa na ubalozi wa Austria wenye ofisi zake nchini Kenya na kwamba endapo lengo la ziara hiyo litafikiwa wakazi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla watanufaika kwa mambo kadhaa ikiwemo ajira.
Mafuru aliongeza kuwa, kama Halmashauri ya Jiji watautembeza msafara huo katika maeneo mbalimbali yaliyopimwa na kutengwa kwa ajili uwekezaji mkubwa ikiwemo wa viwanda ili kuyavutia makampuni hayo kufanya kazi Jijini Dodoma.
Balozi wa Tanzania nchini Kenya Dkt. John Simbachawene alisema kuwa, Tanzania imefarijika kupata ugeni huo ambao unatarajia kufanya uwekezaji kwenye maeneo ya biashara, viwanda, kilimo, nishati, na afya.
Naye afisa Biashara kutoka ubalozi wa Austria Edith Predorf alisema nchi hiyo inapenda kuwekeza Tanzania kwa kuwa kuna fursa nyingi na kwamba suala hilo litaendelea kuimarisha mahusiano mazuri baina ya nchi hizo mbili.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.