MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango leo tarehe 12 Februari, 2022 amezindua Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, uzinduzi uliofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Makamu wa Rais amesema kazi ya kuhifadhi mazingira ikiwemo kulinda vyanzo vya maji, misitu, upandaji miti, kupendezesha miji, kufanya kusafi katika maeneo yote ya makazi na biashara, viwandani na masokoni ni lazima kuanzia sasa kuwa kazi za kudumu. Aidha amesema viongozi wote kuanzia ngazi ya vijiji hadi mikoa wanapaswa kusimamia uhifadhi wa mazingira na suala hilo litakua kipimo cha utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha, Makamu wa Rais amesema ni muhimu kuondoa nadharia katika uhifadhi wa mazingira ikiwemo kuwa na mipango isiyotekelezwa bali inahitajika kazi ya ziada itakayotoa matokeo chanya katika kuhifadhi mazingira. Amesema sheria ndogondogo za uhifadhi wa mazingira zinapaswa kusimamiwa ikiwemo faini na ikiwezekana kuongeza faini hizo ili kukomesha waharibifu wa mazingira. Dkt. Mpango amesema zoezi la kutunza mazingira lazima kuwa shirikishi kwa wadau wote kuanzia mijini na vijijini na kuagiza wizara na taasisi zote za serikali kuhakikisha wanapanda miti na kuitunza katika maeneo yao.
Makamu wa Rais amewataka Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) kutoa elimu kwa wananchi juu ya aina ya miti inayopaswa kupandwa kulingana na maeneo wanayoishi. Aidha amewaasa kuhakikisha wanaongeza miche itakayopandwa ikiwemo kuongeza vitalu katika maeneo mbalimbali ili wananchi wapate urahisi wa kupata miche hiyo.
Vile vile, Makamu wa Rais ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda nchini kuzingatia misingi ya uzalishaji endelevu pamoja na kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira ili kupambana na uchafuzi wa mazingira.
Katika hatua nyingine Makamu wa Rais ameagiza Wizara ya Ardhi, Wizara ya Maji, Wizara ya Kilimo , Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha wanashirikiana kushughulikia suala la uharibifu wa mazingira unaofanywa kwenye chanzo cha mto Ruaha katika Bonde la Ihefu kutokana na kuingizwa kwa makundi makubwa ya mifugo pamoja na kuelekezwa maji katika mashamba makubwa bila kurejeshwa mtoni.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo amesema Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 imezingatia masuala mbalimbali ikiwemo mpango wa taifa wa miaka mitano, mpango endelevu, pamoja na mpango wa miaka 15 ulioanza 2011-2012. Amesema sera hiyo inatarajiwa kuokoa uharibifu wa mazingira katika nchi pamoja na kuongeza fursa za kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa jumla.
Amesema tayari wizara imefanya zoezi la utoaji elimu ya uhifadhi wa mazingira na kuongeza kwamba kwa muda wa siku tano tayari jumla ya miti laki moja na elfu arobaini na moja imepandwa katika jiji la Dodoma pekee huku lengo likiwa ni kupanda miti milioni 14.5 nchi nzima kwa kuwashirikisha wanafunzi nchi nzima.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Marry Maganga amesema maandalizi ya Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 yametokana na kuongezeka kwa changamoto mpya za uharibifu wa mazingira ikiwemo uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka zitokanazo na vifaa vya umeme, matumizi ya kemikali yasioendelevu, mabadiliko ya tabia ya nchi pamoja na changamoto ya shughuli za uchimbaji wa mafuta , madini na gesi.
Naye Mwenyekiti kamati ya kudumu ya Bunge ya Uwekezaji, Viwanda, Biashara na Mazingira David Mwakiposa Kihanzile amesema ni muhimu serikali kuanza haraka mchakato wa kutungia sheria na kanuni sera hiyo ili ianze kutekelezwa kwa ufanisi. Amesema suala la upandaji miti linapaswa kuwa na mkakati maalum utakaorahisisha zoezi hilo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.