HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma inaamini kuwa makao makuu ya nchi yanajengwa na watanzania wote na wawekezaji mbalimbali kwa lengo la kutanua wigo wa ajira na kusogeza huduma kwa wananchi.
Kauli hiyo ilitolewa na kiongozi wa timu ya kimkakati ya Uwekezaji na Masoko ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Leonard Machunde (pichani) katika ukumbi wa Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI) jijini Dar es Salaam.
Machunde alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ndiyo Makao Makuu ya nchi. “Makao makuu ya nchi, hayajengwi tu na wakazi wa Dodoma”. Makao Makuu yanajengwa na watanzania wote na wawekezaji mbalimbali wa ndani na nje ya nchi. Ndiyo sababu halmashauri iliunda timu hii ili ifikishe ujumbe huo kwa Watanzania wote” alisema Machunde.
Akiongelea fursa za uwekezaji zilizopo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Machunde alisema kuwa halmashauri hiyo imetenga eneo la ujenzi wa viwanda Nala. Alisema kuwa eneo hilo lina viwanja vyenye ukumbwa wa kuanzia hekari moja hadi 100. Ujenzi wa viwanda ni fursa muhimu katika kuzalisha ajira,biashara na unachochea usogezaji wa huduma kwa wananchi, aliongeza.
Machunde ambae pia ni mbobezi katika tasnia ya Fedha na Uwekezaji alisema kuwa uwekezaji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni kitendo sahihi. “Bahati nzuri ukinunua kiwanja katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma unakuwa umenunua kiwanja serikalini. Fedha inayolipwa, inalipwa Serikalini kupitia namba ya udhibiti (control number) na hakuna mtu wa kati wa kupandisha gharama. Hivyo, unakuwa katika mikono salama ya serikali” alisema Machunde kwa kujiamini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Maendeleo ya Wanachama na Huduma wa Shirikisho la wenye viwanda Tanzania, Neema Mhondo aliipongeza timu hiyo kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kazi nzuri. Alisema kuwa wawekezaji wanapenda sana kufahamu kama eneo lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji lina miundombinu muhimu ya kuwezesha viwanda kujengwa. Miundombinu hiyo ni umeme, maji na barabara. Alisema kuwa miundombinu hiyo ni muhimu kwa sababu inapunguza gharama za uendeshaji.
Nae Afisa Mipango Miji katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Aisha Masanja alisema kuwa eneo la viwanda Nala lina miundombinu wezeshi na ya uhakika kwa ajili ya ujenzi wa viwanda. Maji na umeme wa msongo mkubwa upo kwa ajili ya viwanda. “Eneo hilo la viwanda Nala lipo kilometa tatu kutoka barabara kuu ya kutoka Dodoma kuelekea Singida na likiwa umbali wa kilometa moja na nusu kutoka barabara ya mzunguko wa nje” alisema Masanja.
Kiongozi wa timu ya kimkakati ya Uwekezaji na Masoko ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Leonard Machunde akifafanua jambo
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Wanachama na Huduma wa Shirikisho la wenye viwanda Tanzania, Neema Mhondo (kulia) akiongea na timu ya kimkakati ya Uwekezaji na Masoko ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika ukumbi wa mikutano wa CTI jijini Dar es Salaam.
Timu ya kimkakati ya Uwekezaji na Masoko ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, ikiongozwa na Leonard Machunde Mpima Ardhi (wapili kushoto). Wa kwanza kushoto ni Ahmed Msangi Mchumi Mwandamizi, Aidha Masanja, Afisa Mipango Miji (wa pili kulia) na Mary Ngowi, Afisa Ardhi (wa kwanza kulia) walipotembelea Shirikisho la wenye viwanda Tanzania (CTI) kuelezea fursa za uwekezaji katika viwanda zilizopo jijini Dodoma
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.