MAKATIBU MAHSUSI nchini wametakiwa kuwa na lugha ya staha wakati wa kutoa huduma kwa umma wakati wa mkutano wao wa mwaka ambapo na Makatibu Mahsusi 3000 wameshiriki Mkutano huo wakiwemo 11 kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Mkutano huo ulifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo ulifunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye aliwakumbusha Makatibu Mahsusi nchini kutumia lugha yenye staha wakati wa kuwahudumia watumishi na wananchi wanaofuata huduma katika taasisi zao.
Wakihojiwa na Tovuti hii ya Jiji kwa nyakati tofauti, Makatibu Muhtasi hao wa Halmashari ya Jiji la Dodoma kila mmoja alikumbusha yale waliyoyapata kwenye mkutano huo ambayo yameamsha ari kubwa kwao kufanya kazi kwa bidii na kusisitiza kauli mbiu ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa ‘Kazi Iendelee’.
Kwa upande wake Joyce Kiula alisema kuwa, “Mhe. Mchengerwa alitukumbusha Makatibu Mahsusi kuwa sisi ni kioo cha ofisi yetu ambapo wageni wanaofuata huduma wanapata taswira halisi ya huduma zinazotolewa na taasisi yetu, hivyo tunapaswa kuwa na kauli nzuri na kutoa huduma bora kwa wageni na wananchi”.
Naye Scola Njawa, ambaye ni Katibu Muhtasi wa Ofisi ya Mweka Hazina wa Jiji la Dodoma, alisema kuwa Mhe. Mchengerwa aliwaambia kuwa hakuna haki isiyokuwa na wajibu. “Kwa msingi huo Waziri ametutaka Makatibu Mahsusi kutofanya kazi kwa mazoea na wale ambao ni kikwazo katika kutoa huduma wabadilike ili kuendana na azma ya Serikali.”
“Mimi kwa upande wangu nilishika sana maneno ya Mhe. Mchengerwa alivyotuasa Makatibu Mahsusi kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia uadilifu hususan utunzaji wa siri za ofisi na akatuonya kuwa watakaobainika kutozingatia taratibu za kazi zetu basi wataondolewa katika ofisi zao” alisema Wankaela Timotheo kutoka ofisi ya Afisa Elimu Sekondari wa Jiji la Dodoma.
Aidha, Maula Komba wa Idara ya Ujenzi alisema kuwa amefurahishwa na kauli ya Mheshimiwa Mchengerwa aliposema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa Makatibu Mahsusi katika uendeshaji wa shughuli za kila siku za ofisi, hivyo hawana budi kuendelea kuilinda imani ya Serikali kwa kuwajibika kikamilifu.
Edina Charles wa Ofisi ya Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika akimkunukuu Mhe. Mchengerwa alisema “Tunahitaji watumishi wachapakazi na waadilifu, kwani dhamira ya serikali ni kusonga mbele, kama utashindwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu utaondolewa bila kujali taasisi uliyopo.” Alisema Edina akionesha kujali sana kauli ya Mhe. Mchengerwa.
Kwa upande wake Fatina Sharifu Katibu Mahsusi wa Mradi wa Uboreshaji Miji wa Kimkakati (TSCP) alisema “Mimi nakumbuka Mhe. Waziri Mchengerwa alihimiza kuhusu uadilifu na alitutaka Makatibu Mahsusi kula kiapo cha Uadilifu kwa Watumishi wa Umma ambapo wote tulitekeleza.
Katika hotuba ya ufunguzi kuna mengi yalisemwa, alianza kuongea Lucy Msigwa Katibu Mahsusi wa Kitengo cha Sheria mojawapo ni suala la waajiri kuthamini umuhimu wa Makatibu Mahsusi wenye umri mkubwa ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya ofisi kwa kutumia uzoefu walio nao ikiwa ni pamoja na uadilifu na uchapakazi wao.
Neema Baseke Katibu Mahsusi ya Idara ya Mipango miji, Ardhi na Maliasiri alisema kuwa “Ili kuendana na Kaulimbiu ya mwaka huu inayohimiza ubunifu, umahiri na uzingatiaji wa weledi katika utendaji kazi kwa Makatibu Mahsusi, tunatakiwa kuitekeleza kwa vitendo kwa kujiendeleza kitaaluma” na Katibu Mahsusi Asia Bwesa alisisitiza kuwa wamejipanga kuyafanyika kazi yale yote waliyoambiwa na kwamba yamewakumbusha wajibu wao na kuamsha ari ya utendaji kazi, "tutajisikia furaha sana kuwa mfano bora kwa wenzetu na kutoa huduma bora kwa wananchi kwa faida ya taasisi yetu na wanaDodoma na wanachi wote kwa ujumla" alimalizia Asia.
Shamimu Makongoro wa Idara ya Utawala alirejea maneno ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella kuhusu umuhimu wa Makatibu Mahsusi kiutendaji kiasi kwamba wakiondolewa hata kwa siku moja, utekelezaji wa majukumu ya taasisi yoyote ile utayumba.
Akiongea na tovuti hii Fatuma Kuchele wa Idara ya Mipango, Takwimu na Ufuatiliaji amesema kada ya Uhazili tunatambua muhimu wetu kwa viongozi na watumishi wengine katika utendaji kazi wa kila siku, na Asia Bwesa akamalizi kuwa “hivyo tunatakiwa kuendelea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ikiwa ni pamoja na kutunza siri za ofisi ili kusukuma gurudumu la maendeleo mbele”.
Chama cha Makatibu Mahsusi Tanzania (TAPSEA) kilianzishwa mwaka 2008 kwa lengo la kukuza na kudumisha taaluma ya Makatibu Mahsusi na kuhimiza uwajibikaji ili kutoa huduma bora kwa umma na mkutano wa mwaka huu wa TAPSEA uliongozwa na kauli mbiu isemayo “Kuwa Mbunifu Mahiri, Zingatia Weledi katika Kuleta Mabadiliko ya Uchumi Tanzania.”
Makatibu Mahsusi wa Jiji la Dodoma wakiwa katika picha ya pamoja waliporejea kwenye kituo chao cha kazi baada ya kuhudhuria mkutano wao mwaka, kutoka kushoto ni Fatuma Kuchele, Joyce Kiula, Scola Njawa, Edina Charles, Asia Bwesa, Neema Baseke na Wankaela Timotheo.
Makatibu Mahsusi wa Jiji la Dodoma wakiwa katika picha ya pamoja kutoka kushoto ni Lucy Msigwa, Fatina Sharifu, Maula Komba, Shamimu Makongoro, Fatuma Kuchele, Joyce Kiula, Scola Njawa na Edina Charles.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.