Makatibu Wakuu na Naibu Makaribu wa wizara tofauti nchini pamoja na sektetarieti ya baraza la mawaziri wakiongozwa na mwakilishi wa Katibu Mkuu kiongozi Mhe. Prof. Sifuni Mchome wametembelea mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa - SGR kipande cha Dodoma - Morogoro jana tarehe 2 Machi 2020.
Lengo la ziara hiyo ya siku mbili yaani tarehe 2-3 ni kuona maendeleo ya mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa – SGR kuanzia Dodoma hadi Dar es Salaam kwa kipande cha Morogoro - Dodoma - Singida chenye urefu wa Kilometa 422 ambao umefikia zaidi ya 28% na Dar es Salaam – Morogoro umbali wa Kilometa 205 ambao umefikia zaidi ya 75%.
Ziara hiyo ilianza Mkoani Dodoma ambapo Makatibu wakiwa na mwenyeji wao Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania - TRC Ndugu Masanja Kungu Kadogosa walitembelea katika maeneo mbalimbali ya mradi ikiwemo kambi kubwa ya mradi wa SGR iliyopo Ihumwa Dodoma, mahahandaki 4 yanayojengwa Kilosa mkoani Morogoro, kiwanda cha uzalishaji wa mataruma chenye uwezo wa kuzalisha mataruma 1100 kwa siku kilichopo eneo la Kilosa pamoja na kuona kazi za ujenzi wa tuta, madaraja, makalavati na uwekaji mataruma, reli na nguzo za umeme kwenye tuta la reli
Akiongea katika ziara hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano sekta ya uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho amesema kuwa Mkandarasi anapiga hatua katika ujenzi na usanifu wa njia ya Reli na kazi kubwa inafanyika usiku na mchana.
“Ziara yetu hii ni ya siku mbili Machi 2 - 3, 2020, leo tumetembelea kipande cha Makutupora hadi Morogoro tumeona kazi kubwa inafanyika kwa kasi katika ujenzi wa mahandaki manne, kesho tutatembelea kipande cha Dar es Salaam – Morogoro, kazi inakwenda vizuri na tunatarajia itakwisha kwa wakati” alisema Chamuriho
Naye mwenyeji wa msafara Mkurugenzi Mkuu wa TRC Masanja Kadogosa amesema kuwa “Sisi kama TRC tunashukuru, ujio huu wa makatibu wa serikali katika mradi huu ambao ni mtambuka ambao unagusa wizara zote, kwahiyo ni ugeni muhimu sana kwa sababu utarahisisha utekelezaji wa mradi huu kwa kuwa watendaji wa wizara tayari watakuwa na uelewa juu ya changamoto na fursa zilizopo katika mradi, hawa ni watu ambao tunafanya nao kazi moja kwa moja”
Aidha Kadogosa amewahakikishia watanzania kuwa mradi wa SGR unaendelea vizuri na utakamilika, “Nawahakikishia watanzania kuwa mradi huu kipande cha Dar es Salaam – Morogoro tumebakisha 25%, hivyo mwaka huu treni lazima itapita na watanzania watapanda kwa mara ya kwanza, tunaendelea vizuri na tuna uhakika 100%” aliongeza Kadogosa.
Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara Prof. Riziki Shemdoe amesema kuwa kitu ambacho amekiona katika mradi wa SGR angetamani kila mtanzania aje aone, kwa kuwa kazi iliyofanyika ni kubwa sana, amemshukuru Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa maamuzi magumu aliyochukua. Ujenzi huu umewanufaisha sana wawekezaji wadogo wadogo, wakulima na wafugaji wakati wa ujenzi na pindi utakapokamilika.
Makatibu hao wameonesha kufurahishwa na maendeleo ya mradi huo na namna ambavyo umesanifiwa kwa kuzingatia mazingira ya kitanzania pamoja na namna ambavyo wananchi wameshirikishwa moja kwa moja katika usanifu na ujenzi wa miundombinu ya reli hiyo ikiwemo vivuko vya magari, wanyama na watembea kwa miguu. Mradi huu utakapokamilika unatarajiwa kuleta manufaa kwa Shirika na uchumi wa taifa kwa ujumla kupitia usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo.
Tazama picha mbalimbali wakati wa ziara hiyo:
Chanzo: Habari na picha kwa msaasa wa Idara ya Habari Maelezo
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.