Na. Dennis Gondwe, DODOMA
WIZARA ya Maliasili na Utalii imeshauriwa kuhamasisha Sensa ya Watu na Makazi ili wananchi wote wahesabiwe kutokana na uzoefu wake katika eneo hilo.
Kauli hiyo ilitolewa na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe alipotembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika maonesho ya wakulima na wafugaji yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.
Prof. Mwamfupe alisema kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii isaidie kuhamasisha Sensa ya Watu na Makazi kutokana na uzoefu wake. “Nasema hili ni muhimu kwenu kwa sababu hata wanyama huwa wanahesabiwa kujua idadi yao na hali ya malisho. Hivyo, ushiriki wenu katika kuhamasisha wananchi kuhesabiwa ni muhimu sana kwa mipango ya maendeleo ya taifa” alisema Prof. Mwamfupe.
Naye mwananchi Sylvester Mwatupasi alisema kuwa kila mtu ana wajibu kuhesabiwa. “Ndugu mwandishi umemsikia hapa Meya wakati akiongelea wizara inavyohesabu wanyama kujua idadi yao, hiyo ndiyo sensa. Kama wanyama wanahesabiwa, je sisi binadamu kitakachofanya tusihesabiwe ni nini! Ni wajibu wetu kwa umoja wetu tushiriki zoezi hili kwa umakini kama unavyosisitizwa ili tuwe sehemu ya kufanikisha mipango ya serikali” alisema Mwatupasi.
Maonesho ya shughuli za Kilimo na Mifugo mwaka 2022 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Agenda 10/30: kilimo ni biashara, shiriki kuhesabiwa kwa mipango bora ya kilimo, mifugo na uvuvi”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.