WANANCHI wametakiwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika vituo vya uandikishaji na siku ya kupiga kura ili kuchagua viongozi wanaoendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Kauli hiyo ya hamasa imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan muda mfupi baada ya kujiandikisha katika kituo cha Shule ya msingi Dodoma Mlimani, iliyopo katika Mtaa Salimin, Kata ya Tambukareli jijini Dodoma leo asubuhi.
Mama Samia amewaomba wananchi wote kujitokeza na kujiandikisha katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019. Amewataka pia kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura ili kuchagua viongozi watakaowasimamia katika mitaa yao. “Mimi nimekuja kujiandikisha kwa sababu makazi yangu ni hapa Dodoma, na hawa ndio watanisimamia mambo yangu” amesema Mama Samia. Aidha, amewataka wananchi kuchagua viongozi wenye maadili mema na watakaowatumikia watanzania na kutunza rasilimali za nchi. Sifa nyingine za viongozi watakaochanguliwa alizitaja kuwa ni dhamira ya kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi na kwenda na kasi ya Serikali ya awamu ya tano.
Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge alisema kuwa Mkoa wa Dodoma unatarajia kuandikisha wananchi 900,000, ukiwa na vituo 3,679. Alisema kuwa siku ya kwanza ya uandikishaji tarehe 8 Oktoba, 2019 jumla ya wananchi 156,000 waliandikishwa.
Uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 utafanyika tarehe 14 Novemba, 2019 ukiongozwa na kaulimbiu isemayo “Viongozi bora wa Serikali za Mitaa ni chachu ya maendeleo, ni haki na wajibu wako kujiandikisha, kugombea na kuchagua kiongozi kiongozi bora”.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suhulu Hassan (katikati) akizungumza na waandishi wa habari mara tu baada ya kujiandikisha kwenye Daftari la Wapiga kura Jijini Dodoma leo. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Binilith Mahenge na kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi wa Jiji la Dodoma Hidaya Maeda.
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suhulu Hassan akipata maelezo kutoka kwa Mwandikishaji wapiga kura wa Mtaa wa Salimini, Kituo cha Shule ya Msingi Dodoma Mlimani bi. Asha Bakina Mussa leo Jijini Dodoma kabla Mama Samia hajajiandikisha kwenye Daftari la Wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.