Na.Coletha Charles, Dodoma
MAMIA ya wafanyakazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameuaga mwili wa aliyekuwa Mtumishi mwenzao dereva Daraja la II Karim Shabani, katika viwanja vya Manispaa ya zamani kilichotokea tarehe 13 Januari, 2025.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji, Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Joseph Fungo, aliwataka watumishi kuishi kwa namna inavyompendeza Mungu , kufanya kazi kwa bidii na uaminifu ili siku zao zikikoma za kuishi duniani Mwenyezi Mungu akawalipe thawabu kwa mema waliyoyafanya.
Alisema kuwa watumishi wasifanye vitu ambavyo havipo kwenye miongozo ya kazi zao ili wasijitengenezee hukumu kwa Mwenyezi Mungu na badala yake, kufanya kazi kwa bidii ili iwe sadaka. “Tumejifunza kwenye vitabu vya dini sisi hapa duniani, kama alivyosema mchungaji maisha yetu ni mafupi na yamejaa shida na tabu, Lakini baada ya maisha haya tunatarajia kwenda mbinguni kila mtu anatamani kufika mbinguni. Wakati mwingine kinachotatiza ni njia ya kwenda mbinguni na hiki kilichotokea kwa mwenzetu leo ndiyo njia ya kwenda mbinguni” alisema Fungo.
Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la Anglikana, Hephice Mlulu, aliyeongoza ibada ya kumuaga marehemu, aliwakumbusha waombolezaji na wafanyakazi kuwa, changamoto zozote wanazopitia zisiwatenge na Mungu kwa sababu ni kimbilio wakati wa tabu.
Alisema kuwa mwanadamu ana moyo mwepesi anapoguswa na jambo kama hili moyo wake lazima utikisike na kushtuka ambapo siku za mwanandamu za kuishi zimekwisha kuhesabiwa na si nyingi. “Mungu anasema hivi vyote vitatoweshwa kama kivuli, kama tunavyoona maisha ya ndugu yetu alistawi na alichanua, matumaini yetu sote alikuwa ni nguvu kazi ya taifa katika ofisi. Lakini Mungu alisema hapana, siku zake zimekoma, na Yesu alisema yeye ndiye njia ya kweli na uzima, zipo njia za mikato lakini kifo hakina hiyo njia” alisema Mlulu.
Mwili wa marehemu Karim Shabani umesafirishwa kwa ajili ya kupumzishwa huko Mkoani Kigoma, Wilaya ya Kibondo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.