WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amesema, shilingi Milioni 264.3 zilizotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) zimetumika kujenga zahanati ya Kijiji cha Ikelu iliyopo katika Halmashauri ya Mji Makambako na nyumba ya watumishi wa zahanati hiyo ili kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.
Mhagama amesema hayo, mara baada ya kukagua ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Ikelu na nyumba ya watumishi wa zahanati hiyo, akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika Halmashauri ya Mji Makambako.
Mhagama amesema kuwa, kutokana na maombi ya wananchi wa Kijiji cha Ikelu, Rais Samia Suluhu Hassan kwa mapenzi yake aliridhia milioni 264.3 zitumike kutatua changamoto ya kukosekana kwa huduma za afya kwa wananchi wa kijiji hicho.
"Rais kupitia fedha za TASAF alielekeza ijengwe zahanati na nyumba ya watumishi wa zahanati hiyo ili kuondoa tatizo la ukosefu wa zahanati na nyumba ya watumishi wa afya ambao wana jukumu la kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora itakayowawezesha kushiriki shughuli mbalimbali za maendeleo," Jenista amefafanua.
Akizungumzia ubora wa zahanati na nyumba ya watumishi iliyojengwa, Mhagama amesema kuwa amekagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo wa zahanati na nyumba hiyo ya watumishi, na kubaini kuwa miradi yote miwili imejengwa kwa ubora na viwango vinavyotakiwa kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyotumika.
Sanjari na hilo Mhagama amesema, Serikali haitoishia katika ujenzi wa zahanati na nyumba ya watumishi pekee kwani Rais ameiagiza TASAF kuleta vifaa tiba ili kuhakikisha huduma ya afya ya mama na mtoto pamoja na wananchi kwa ujumla zinapewa kipaumbe kama ambavyo Serikali ya Awamu ya Sita imekusudia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Kissa Kasongwa amesema wananchi wa Kijiji cha Ikelu wanamshukuru Rais kwa kuwajengea zahanati.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.