HALMASHAURI ya Manispaa ya Dodoma imeanza utekelezaji wa agizo la Serikali la kila Halmashauri nchini kuhakikisha inaangamiza vimelea vya mbu waenezao ugonjwa wa Malaria kwa kupulizia dawa katika maeneo yote ambayo ni rafiki kwa vimelea hivyo kukua.
Utekelezaji wa agizo hilo umeanza jana Jumanne Desemba 12, 2017 na litadumu kwa siku saba, ambapo watakaohusika na upuliziaji ni watumishi sita (6) kutoka Ngazi ya Halmashauri na Wanajamii sitini (60) wa kujitolea kutoka katika Kata 41 za Manispaa ya Dodoma.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma Hamad Nyembea amesema maeneo ambayo yatapuliziwa dawa kwa ajili ya kushambulia vimelea hivyo ni pamoja na maeneo ya Mabwawa yakiwemo mabwawa ya Maji Taka, madimbwi yanayotuamisha maji, makorongo, mifereji, na matenki yanayotumika kuhifadhia maji majumbani.
Zoezi hili ni shirikishi ambapo ngazi zote za uongozi katika Wilaya zitashiriki kwa namna moja au nyingine katika usimamizi, kuanzia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Madiwani, Menejimenti ya Halmashauri, Timu ya Uendeshaji wa Huduma za Afya ya Halmashauri, Viongozi wa Tarafa, Kata, Mitaa, Vijiji na Vitongoji.
Kwa Mujibu wa Daktari Nyembea, dawa inayopuliziwa ni mahususi kwa ajili ya kushambulia vimelea vya mazalia ya Mbu tu, na haina madhara yeyote kwa binadamu hivyo amewataka wakazi wa Manispaa kutokuwa na hofu yeyote kwani zoezi hili ni muendelezo wa vita ya muda mrefu ya kutokomeza ugonjwa wa Malaria nchini.
Alitoa wito kwa Wananchi kuwa watulivu na kutoa ushirikiano utakaohitajika wakati wa zoezi la upuliziaji, ambapo wadau mbalimbali pia watashirikishwa ikiwemo Vyombo Vya Habari, Viongozi wa Dini, Watu maarufu, na Taasisi mbalimbali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.