HALMASHAURI ya Manispaa ya Iringa inajipanga kuanza kufanya uwekezaji mkubwa katika Jiji la Dodoma kwa lengo la kuongeza mapato yake na kukuza utoaji wa huduma kwa wananchi wake.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Hamid Njovu alipokuwa akiongea na timu ya wataalam wa kutangaza fursa za uwekezaji kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma walipomtembelea ofisini kwake kuishawishi manispaa yake kuwekeza Dodoma.
Njovu aliishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kupanga ziara ya kuhamasisha wawekezaji wa Manispaa ya Iringa kuwekeza jijini Dodoma. “Kwetu kama Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na kwangu kama Mkurugenzi wa Manispaa nimeona ni jambo zuri na nimeomba andiko pamoja na wasilisho lenu ambavyo nitaviwasilisha kwenye timu yangu ya wataalam kwa lengo la kuhakikisha wataalam wetu wanafikiria tofauti, kwamba sisi tunaweza kuwekeza katika Jiji la Dodoma” alisema Njovu.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa ni wakati muafaka kwa Manispaa ya Iringa ikajenga hoteli katika Jiji la Dodoma. “Ni vizuri sana tukawa na hoteli katika Jiji la Dodoma ili tunapotengeneza mnyororo wa watalii wetu watoke Dodoma waje Iringa, kwenda katika Hifadhi ya taifa ya Ruaha na maeneo mengine ya vivutio iwe rahisi zaidi. Kwangu mimi, nazishauri sana Halmashauri, kuna Halmashauri za Wilaya au Halmashauri za Miji zina mapato makubwa sana, lakini uwezo wao wa mapato upo katika mazao ya kudumu au mazao ya biashara. Ni muda sahihi wa kufikiria kubadilisha uwekezaji na kuhama na kuwekeza Dodoma, tusitegemee haya mazao na ushuru tuliouzoea wa masoko, ipo siku tunaweza kuachana na ushuru huo” alisema Mkurugenzi Njovu.
Awali akielezea fursa za uwekezaji zilizopo jijini Dodoma, Afisa Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Zainab Manyike alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma imepima viwanja katika maeneo ya kimkakati kwa ajili ya matumizi mbalimbali. Viwanja hivyo vipo kwa ajili ya ujenzi wa hoteli vinavyopatikana katika maeneo ya Mtumba, Iyumbu, Njedengwa na Kitelela, aliongeza. “Vipo viwanja kwa ajili ya ujenzi wa taasisi mbalimbali za serikali na binafsi katika eneo la Mtumba, Nala, Kikombo, Iyumbu, Nzuguni, Chahwa na Kitelela. Mkurugenzi nikwambie tu, hata Halmashauri ya Jiji la Dodoma inajenga hoteli yake ya ghorofa 11 kwa mapato ya ndani ikiwa katika hatua za mwisho kukamilika. Hivyo, Manispaa yako pia inaweza kwenda kujenga hoteli katika Jiji la Dodoma na kuongeza mapato yake. Na bahati nzuri, viwanja hivi vipo Halmashauri na hakuna dalali” alisisitiza Manyike kwa kujiamini.
Halmashauri ya Jiji la Dodoma imeamua kutoka ofisini na kuwafuata wawekezaji katika maeneo yao kuelezea fursa zilizopo kwa lengo la kuwavutia kuwekeza jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Hamid Njovu (kushoto) akielezea mpango wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuwekeza Jijini Dodoma mbele ya timu ya wataalam wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Afisa Ardhi Nuru Maliki (kulia) na Afisa Maendeleo ya Jamii Zainabu Manyike (katikati) ofisini kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.