HALMASHAURI ya jiji la Dodoma imezindua mfumo rasmi kwa njia ya mtandao ambao utatumika kila mwananchi kujaza fomu ya maombi ya kupata kibanda cha biashara katika miradi ya soko kuu la Job Ndugai pamoja na stendi kuu iliyopo Nzyuguni ikiwa ni jitihada za kupambana na ugonjwa wa COVID-19.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi wa Jiji hilo Godwini Kunambi leo wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mfumo huo pamoja na taratibu zitakazo fuatwa na wananchi katika kufanikisha zoezi hilo.
Kunambi alisema kuwa mfumo huo umeandaliwa na wataalamu kwa ufanisi mkubwa ambapo utawapa fursa watu wote waliopo ndani na nje ya Mkoa wa Dodoma , kujaza fomu ya maombi kwa kutumia simu ya mkononi yenye mtandao au kompyuta huku akiwaahidi wananchi wote ambao walilipia fomu ya maombi shilingi elfu ishirini kuwa watarudishiwa fedha zao kwani zoezi hilo linaanza upya na halilipiwi.
Alisema mfumo huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa msongamano wa watu ambao ungesababisha maambukizo ya ugonjwa huo wa Corona, kila mwananchi kupata fursa ya kupata kibanda, kuondoa lawama pamoja na kuondokana na adha ya kusafiri kuja Dodoma badala yake watafuata utaratibu unaotakiwa ili kufanikiwa zoezi hilo.
"Jiji kwa kushirikiana na wataalamu mbalimbali wa Serikali na ofsi ya mkuu wa Mkoa imeandaa mfumo huu ambao tumefanikiwa na leo tunauzindua na unaanza rasmi kutumika ambapo tunatoa fursa kwa watu wote bila kujali dini, cheo wala umaarufu, kuanza kutumia mfumo huu kuomba na kujaza fomu kwa ajili ya kupata kibanda cha biashara katika soko kuu la Job Ndugai na Stendi kuu mpya ndani ya siku saba ambapo jumla miradi yote miwili itahitaji waombaji 1000 ."alisema Kunambi
"Na niwataarifu watanzania kwamba kila mmoja anayo fursa ya kuomba na kufuata vigezo vyote ambavyo vitaoneshwa kwenye mtandao wakati wa kujaza fomu bila kusahau kuambatanisha leseni ya biashara ambapo baada ya kujaza mtandao wenyewe utafanya upembuzi kwa ambao watatimiza masharti hivyo sitegemei lawama zozote kwani mimi na timu yangu hatuna mamlaka yoyote mtandao utafanya kila kitu"alisema Kunambi
Aidha alisema kutokana na miradi mikubwa minne iliyopo, kuna miradi miwili ya mapumziko na sehemu ya kupaki malori haitaombwa kwa njia ya mtandao bali itatangazwa kwenye zabuni ambapo kutakuwa na utaratibu wake.
"Na pia niwafafunulie kwamba muombaji anatakiwa kuwa na namba ya usajili (TIN), leseni hai ya biashara, kitambulisho cha utaifa (NIDA), awe na kompyuta au simu yenye mtandao wa intaneti "aliongeza Kunambi.
Hata hivyo aliwataka machinga kutokuomba kupitia mfumo huo kwani kuna utaratibu na eneo maalumu ambao umewekwa kwa ajili yao.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.