WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo ametoa wito wa kutumia maarifa yanayopatikana katika maonesho ya Nanenane mwaka 2020 kuleta mabadiliko yenye tija katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Kauli hiyo aliitoa wakati akifungua maonesho ya Nanenane kanda ya kati yanayoendelea katika uwanja wa Nanenane Nzuguni jijini Dodoma.
Waziri Jafo alisema “tuna kila sababu ya kujitathmini, maonesho haya yanafanyika kila mwaka, bado tuna fursa kubwa tulizokuwa nazo ila hatujatumia vya kutosha fursa hizi. Leo ukienda Kongwa, Mpwapwa, Manyoni, Itigi, Mkalama, Bahi, mimi imani yangu kama mafunzo yanayotolewa hapa yakitumika kwa 75% tutapata mafanikio makubwa sana katika uchumi wetu. Imani yangu bado maarifa hayajatumika kwa asilimia kubwa”. Maarifa hayo yakifanyiwa kazi katika miaka mitano ijayo itaifanya nchi kuingia katika uchumi wa kati uliyoendelea kuimarika zaidi, aliongeza.
Alisema kuwa maarifa hayo yanatakiwa kupelekwa katika utendaji zaidi kutoka katika dhana ya maonesho na kwenda katika dhana ya utekelezaji kivitendo. “Lakini fahamu nchi yetu tupo katika eneo la kimkakati kijiografia. Ni miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, tupo ukanda wa SADC, tunafursa ya kujenga uchumi wetu kupitia kilimo, mifugo na uvuvi” alisema Waziri Jafo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.