WALIMU wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wameshauriwa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 unaosababishwa na virusi vya Korona ikiwa ni pamoja na kuchanja ili kujihakikishia usalama na kuwalinda wanaowapenda.
Ushauri huo ulitolewa jana na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method alipokuwa akiongea na maelfu ya walimu wa halmashauri hiyo katika uwanja wa Jamhuri jijini hapa.
Dkt. Method alisema kuwa ugonjwa wa UVIKO-19 upo katika Jiji la Dodoma na njia za kukabiliana nao ni kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kuvaa barakoa na kuachiana nafasi. “Ndugu zangu pamoja na njia hizo, tunayo chanjo ya ugonjwa huo. Tumeshuhudia ndugu zetu wakiugua ugonjwa huu na kufariki. Tumeshuhudia vifo vya watumishi na marafiki zetu. Kuna vifo vya watumishi wa Afya vilivyotokana na wao kuwahudumia wagonjwa wa UVIKO-19. Tumeshuhudia vifo vingi vya walimu wetu kutokana na kutekeleza majukumu yao” alisema Dkt. Method kwa uchungu.
Mganga Mkuu huyo alisema kuwa uongozi wa wilaya umewaita ili kuwapa fursa ya kupata elimu sahihi ya chanjo ya ugonjwa huo. “Ndugu zangu kutokana na umuhimu wenu katika jamii, na nafasi yenu kama walimu, tunawapa elimu hii ili nanyi muwe na uelewa na mpate nafasi ya kuuliza maswali na sisi tutayajibu ili kuondoa sintofahamu iliyopo katika jamii. Nataka niwaambie ‘experience’ ya kuugua UVIKO-19 siyo nzuri. Tusithubutu kutaka kuugua ugonjwa huo ili tufanye maamuzi” alisema Dkt. Method kwa sauti ya tahadhari.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Joseph Mabeyo alisema kuwa kundi la walimu ni muhimu katika mustakabali wa elimu katika Jiji la Dodoma. Alisema kuwa hiyo ni fursa kubwa kwao kusikiliza kwa makini na kuuliza maswali ambayo yatawasaidia kuelewa zaidi juu ya ugonjwa wa UVIKO-19.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Dkt. Andrew Method (aliyesimama) alipokuwa akiongea na maelfu ya walimu wa halmashauri hiyo katika uwanja wa Jamhuri jijini hapa. Kushoto ni Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rweyemamu.
Afisa Elimu Msingi Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Joseph Mabeyo alipokuwa akiongea na walimu wa Jiji la Dodoma katika uwanja wa Jamhuri.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.