Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amepiga marufuku hospitali nchini kuzuia maiti kutokana na gharama za matibabu na badala yake zibuni njia mbadala za kudai malipo hayo.
Katazo hilo alilitoa jana jijini Dar es Salaam, alipofanya ziara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Tawi la Mloganzila, kuangalia kero na vikwazo wanavyopata wagonjwa wanaopatiwa matibabu.
Alisema anafahamu lipo tatizo la wananchi kushindwa kumudu gharama za matibabu na ikizingatiwa kuwa hospitali hiyo inatoa huduma kwanza kabla ya kudai malipo.
"Ni marufuku hospitali kuzuia maiti kwa sababu mgonjwa alishindwa kulipa deni. Watafute utaratibu mwingine wa deni kulipwa bila kuzuia maiti," aliagiza.
Ummy alitoa agizo hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wagojwa wanaodaiwa hospitalini hapo baada ya kupatiwa matibabu na hali zao kuimarika.
Alisema hilo ni tatizo katika hospitali nyingi nchini na kwamba serikali inafanyia kazi kuhusu namna ya kuwezesha wananchi wote kupata huduma za matibabu.
Waziri huyo alisema wameshatoa mapendekezo serikalini kuhusu bima ya matibabu kwa wote, lakini serikali imechelewa kutoa majibu kwa sababu wanafanya tathmini ya gharama ambayo kila Mtanzania atamudu na mfuko utatoa huduma.
"Suala la wananchi kushindwa kumudu gharama za matibabu siyo hapa tu, ni la nchi nzima, ni changamoto (tatizo) ambayo serikali inaifanyia kazi, nasi kama wizara tushatoa mapendekezo yetu, serikali imechelewa kutoa uamuzi kwa sababu lazima tufanye tathimini kuhusu gharama na matibabu," alisema.
Alisisitiza kuwa licha ya kuwapo kwa tatizo hilo, wananchi hawapaswi kunyimwa huduma za matibabu wala maiti kuzuiwa.
Mbali na tatizo hilo, Ummy alisema hospitali hiyo pia iko mbali na makazi ya wananchi, akiahidi kuwa suala hilo linafanyiwa kazi na Manispaa ya Ubungo ambayo inajenga kituo cha mabasi kwa lengo la kurahisisha usafiri.
Alisema wingi wa ndugu wa wagonjwa wanaokwenda hospitalini hapo kuona wagonjwa ni tatizo lingine kulingana na miundombinu ya jengo la hospitali hiyo, inayowalazimu kupanda lifti.
"Najua ipo changamoto ya ndugu kulalamika kukaa foleni muda mrefu kusubiri kuwaona wagonjwa wa hii inatokana na miundombinu ya jengo letu hili, lilijengwa kwa mfumo wa nchi za wenzetu ambao watu wawili au watatu huenda kuona wagonjwa.
"Lakini hapa kwetu mgonjwa mmoja wanaenda ndugu 10 hadi 20 kumtizama na hatuwezi kusema tuwazuie kwa sababu ndiyo utamaduni wetu.
"Naomba angalieni mpeane zamu, ndugu wote hawawezi kupanda lifti kwa wakati mmoja, ndiyo sababu kuna changamoto hii," alibainisha.
Kuhusu huduma za matibabu zinazotolewa hospitalini hapo, Waziri Ummy alikanusha taarifa kuwa wanaotibu wagonjwa ni madaktari wanafunzi waliopo mafunzoni.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Lawrence Museru, alisema sababu ya kuwapo kwa kashfa ya kuwa hospitali hiyo haina madaktari na wagonjwa wanafariki dunia, ilitokana na mfumo wa awali ulioitambulisha hospitali hiyo kama kituo cha mafunzo kwa wanafunzi wa udaktari.
"Hiyo ni dhana ambayo ilijengeka kwa wananchi, lakini tangu imekuwa hospitali ya MNH, hakuna changamoto hiyo na kuna madaktari bingwa wanaotoa huduma," alisema.
Chanzo: www.ippmedia.com
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.