WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa amepiga marufuku walimu kupita kila Ofisi ya Halmashauri kutafuta huduma na ameagiza wapelekewe huduma hizo shuleni badala ya watoa huduma kufuatwa ofisini.
Ametoa agizo hilo leo tarehe 8 Septemba, 2022 Jijini Dodoma wakati akiongea na waandishi wa habari kutoa taarifa kwa umma ya uboreshaji wa huduma kwa walimu nchini.
“Ni marufuku kuwaacha walimu kupita kila ofisi ya Halmashauri kutafuta huduma, narudia tena mwalimu apelekewe huduma shuleni badala ya watoa huduma kukaa ofisini” amesema Bashungwa.
Amesisitiza kuwa Mwalimu akiandika barua kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhitaji huduma, anapaswa kujibiwa kwa maandishi ndani ya siku 7 baada ya kupokelewa.
Aidha, Bashungwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kuwasimamia Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Maafisa elimu, Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu na Wathibiti Ubora wa Shule kuhakikisha wanawafuata walimu mashuleni na kutatua kero na malalamiko yao kwa wakati.
Amewataka viongozi hao kufuatilia na kuwasimamia viongozi wa elimu katika ngazi ya Mikoa, Halmashauri, Kata na shule kutekeleza mikakati ya uboreshaji na usimamizi wa elimu na kuhakikisha wanawasilisha taarifa ya utekelezaji Ofisi ya Rais – TAMISEMI kila robo mwaka.
Vile vile, amewataka kusimamia utekelezaji wa Mipango ya Mafunzo kazini kwa walimu, kwa mujibu wa Mwongozo uliotolewa na Katibu Mkuu Utumishi na ufanyike kwa uwazi na ushirikishwaji wa kutosha, ili kuondoa dhana ya kuwa waajiri wanatoa nafasi za mafunzo kwa upendeleo.
Pia, Bashungwa amewaelekeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwasimamia Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu kuzingatia miongozo ya upandishwaji vyeo walimu, ili kila anayestahili kupandishwa cheo, anapandishwa kwa mujibu Sheria, Kanuni na Miongozo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.