MATUMIZI sahihi ya digitali kwa mtoto wa kike yatachochea maendeleo endelevu kupitia nyanja za elimu, biashara, habari na mawasiliano nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Aziza Mumba katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani yaliyofanyika ngazi ya wilaya katika Kata ya Nkuhungu jijini Dodoma.
Mumba alisema kuwa matumizi sahihi ya digitali kwa mtoto wa kike yatachochea maendeleo katika nyanja za elimu, biashara, siasa, habari na mawasiliano. “Hii itapelekea maendeleo endelevu katika jamii kwa kupata wataalam wa nyanja mbalimbali na pia kuzalisha ajira rasmi na zisizo rasmi. Hali hii itachochea mtoto wa kike kujiongezea kipato na kuwajengea uwezo, ujasiri katika kufanya maamuzi sahihi. Ikumbukwe kwamba mtoto wa kike ni mama mtarajiwa hivyo, kumjengea uwezo wa kujiamini ni kujenga jamii inayojiamini na kujisimamia” alisema Mumba.
Mwakilishi huyo wa Katibu Tawala wa Mkoa, ambae pia ni Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia sekta ya Uchumi na Uzalishaji katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alisema matumizi sahihi ya digitali yamlinde mtoto dhidi ya madhara yanayoweza kutokea. “Nitoe rai kwa jamii kutumia vizuri digitali ili kumwepusha mtoto wa kike na madhara yanayoweza kutokea iwapo haitatumika vizuri. Madhara hayo ni kama unyanyasaji wa kijinsia, mimba za utotoni, kutumia muda mwingi katika vyombo vya kidigitali na kushindwa kuzalisha na pia kumomonyoka kwa maadili katika jamii” alisema Mumba.
Aidha, aliwataka kuzipuuza mila na tamaduni za kigeni ambazo ni kinyume na maadili ya kitanzania na kuwataka kudumisha mila nzuri za kitanzania zinazolinda heshima, utu na ubinadamu. “Maana siku hizi kumeibuka tabia za kuiga katika mitandao ya kijamii mambo yasiyofaa na yenye kudhalilisha utu na ubinadamu wetu. Tabia hizi tuachane nazo kwa sababu hazitusaidii na badala yake zinasababisha mmommonyoko wa maadili katika taifa” alisema Mumba.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa idara ya Maendeleo ya Jamii na Vijana, Asha Vuai alisema kuwa lengo la maadhimisho hayo ni kuwaelimisha na kuwakumbusha wazazi umuhimu wa mtoto wa kike katika kipindi hiki cha kidigitali.
“Kama ujumbe unavyosema ‘Kizazi cha Kidigitali ni kizazi chetu’ Tutumie vifaa vya TEHAMA kwa lengo la kuelimisha watoto kama kufanya ‘homework’ na kujifunza. Tuangalie watoto wanapojifundisha ili wasijifundishe mambo ya ajabu. Tunaona mimba za utotoni zimekuwa tatizo kubwa sababu ni watoto wanajifundisha mambo mabaya kupitia TEHAMA” alisema Viai.
Aidha, aliwataka wazazi kuhakikisha wanawalea watoto wao na kuwa nao makini ili TEHAMA iwe msaada katika kuwafundisha na kuwalea watoto.
Maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike duniani yamefanyika ngazi ya wilaya ya Dodoma katika Kata ya Nkuhungu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.