Wakazi wa Kata ya Chahwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kuhakikisha wanawapeleka watoto shule kupata elimu kwani elimu ndio mkombozi wa maisha yao, lakini pia kutailetea Kata hiyo maendeleo pamoja na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira, na Wenye ulemavu Mhe. Anthony Peter Mavunde alipokua akikabidhi vifaa vya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Chawa, ambayo imeanza kujengwa kwa nguvu za wananchi wa Kata hiyo, vifaa hivyo ni pamoja na mifuko 100 ya saruji, mchanga trip 6 na kokoto trip 3 huku akiahidi kutoa tofali elfu tano ili kufanikisha ujenzi huo, Mavunde amefanya hili ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa baada ya wananchi wa kuwasilisha maombi yao kwenye mkutano wa hadhara wa kampeni alipokuwa akisikiliza kero za wananchi mwezi Januari 2020.
Mavunde amewapongeza wananchi hao kwa kujitoa, na kuamua kutumia nguvu zao kuanzisha ujenzi wa Sekondari hiyo, na yeye yupo tayari kuwasaidia kuona malengo yao yanatimia, na amewahakikishia kuwa mpaka kufikia Mwaka 2021 atakua amesimamamisha moja ya majengo ya Shule hiyo na wanafunzi wataanza kulitumia.
“Shule hii ni ya Wananchi, sitaki ionekane kuwa ni ya Mbunge, shule hii ni ya kwenu, nyinyi ndio wahusika wakubwa, muipende, muijali na msaidie kila hatua, mimi kazi yangu ni kuchochea maenedeleo tu lakini shule hii ni ya kwenu, kila mtu achangie hata kama una elfu tano usiione ndogo inaweza kusaidia kufanikisha ujenzi wa shule hii, Leo tunaandika historia mpya kwa kuanza kutatua kero ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule” alisema Mavunde.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Diwani aliyemaliza muda wake Mhe. Sospeter Mazengo amemshukuru Mhe. Mavunde kwa mchango mkubwa alioutoa katika ujenzi wa shule hiyo na kuwa historia itamkumbuka kwa kuchochea maendeleo kupitia elimu ambapo shule hii itawasaidia wanafunzi wengi wanaotembea umbali mrefu kwa sasa ili kupata elimu kwa kusoma katika kata za jirani.
Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari Mwl. Happy Rweyemamu amewashukuru wananchi hao kwa kujitoa kwani wameonesha ni jinsi gani wanathamini elimu na wao kama Serikali wapo tayari kuwaunga mkono kwa kila namna kuhakikisha shule hiyo inakamilika.
“Ninajua kiu yenu kwasababu nimesikia kwenye ripoti iliyosomwa hapa, kuwa mnatamani 2021 wanafunzi wawe wameanza kuitumia shule hii, mimi kama kiongozi ninaesimamia elimu ya sekondari nitahakikisha shule hii inasajiliwa na inaanza kama nyinyi mnavyotamani iwe, pia nichukue nafasi hii kumpongeza Mhe. Mbunge, niwahakikishie tuna mbunge mzuri mchapakazi anaejituma na kujali wananchi wake” alisisitiza Mwl. Rweyemamu.
Mheshimiwa Anthony Mavunde (katikati) akifurahia jambo na Mkuu wa Idara ya Elimu ya Sekondari Upendo Rweyemamu wakati alipokuwa akikabishi vifaa mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari katika Kata ya Chahwa. Kulia ni aliyekuwa Diwani wa Kata ya Chahwa kabla ya kuvunjwa rasmi Mhe. Sospeter Mazengo.
Mhe. Mavunde akishiriki kazi ya kuchimba msingi wa darasa la shule ya sekondari inayojengwa.
Diwani aliyemaliza muda wake Mhe. Sospeter Mazengo akishiriki kuchimba msingi wa ujenzi wa majengo ya shule ya sekondari.
Mifuko 100 ya saruji iliyotolewa na Mhe. Mavunde ikishushwa kutoka kwenye gari.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.