Mbunge wa Dodoma mjini ambaye pia ni Naibu Waziri ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, kazi, vijana na Ajira, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Wenye ulemavu Mhe. Anthony Mavunde amesema kufikia 2021 shule zote za msingi jijini Dodoma zitakuwa zimepatiwa umeme ili kuweza kutumia kompyuta katika kuboresha sekta ya elimu kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya tano.
Kauli hiyo aliitoa jana katika Uzinduzi wa shule shikizi ya Msingi Chiwondo iliyojengwa kwa msaada wake akishirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambapo tayari vyumba vinne vya madarasa vimeshakamilika huku vingine vitatu vikiwa kwenye hatua ya ujenzi.
Aidha, Mhe. Mavunde alisema serikali imetenga billion 50 ili kuweza kukamilisha usambazaji wa umeme katika maeneo yaliyobaki bila kupatiwa umeme.
“Kwa shule zilizobaki bila kupatiwa umeme nitahakikisha kabla ya mwaka huu 2020 haujaisha wanapatiwa umeme ili pia waweze kupatiwa kompyuta zitakazo wafanya kunufaika na elimu bora wanayotakiwa kupata watoto wetu wa kitanzania” alisema Mavunde
Mavunde aliongeza kuwa uchimbaji wa visima vya maji 13 pia unaendelea na katika visima hivyo kata ya Nala nao ni miongoni mwa wanufahika wa visima hivyo lengo likiwa ni kuwapatia wananchi wake huduma ya maji safi na salama.
Akizungumza mbele ya mgeni rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo, Mhe. Mavunde alisema kuwa anatambua juhudi za OR-TAMISEMI katika sekta ya elimu hivyo anaunga mkono juhudi hizo kwa kukarabati miundombinu ya elimu ili kuhakikisha elimu bora inapatikana kwa kila mtanzania.
Vilevile, aliwataka wananchi wa kata ya Nala kutunza miundo mbinu na kutoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ya kuwasaidia ili waje kulitumikia taifa lao wakati ukifika.
Mavunde alisema kuwa ujenzi wa shule hiyo utasaidia kupunguza kero kwa watoto na wananchi wa kata hiyo kwani awali walitembea mwendo mrefu wa kilomita 20 kwenda shule iliyokuwa mbali.
Akikazia katika hilo, Waziri Jafo amemwagiza Mkurugenzi wa Elimu OR-TAMISEMI, Bw. Julius Nestory kabla ya mwezi wa sita mwaka huu awe amepeleka fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa ili ifikapo mwakani 2021 wanafunzi wote wawe wameacha kutembea umbali wa mwendo mrefu kufuata elimu.
“Mkurugenzi wa Elimu OR-TAMISEMI hakikisha katika ajira zitakazotoka, shule hii inapewa kipaumbele cha kupatiwa walimu kwani mwakani wanafunzi wote wanaotembea mwendo mrefu kufuata elimu watakuwa wamehamia katika shule hii ya Chiwondo.
Awali Mkurugenzi wa jiji la Dodoma Godwini Kunambi alisema kuwa ametoa pikipiki mbili kwa walimu wawili wanao hudumu katika shule hiyo huku akiweka wazi kuwa ofisi yake inaweka utaratibu mzuri wa kuweza kuwajengea nyumba za kuishi walimu hao na kuepuka adha ya kutembea mwendo mrefu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge alitoa wito kwa wazazi na walezi wa wanafunzi kutoa ushirikiano kwa kuhakikisha wanafunzi wanafika shuleni na kuendelea kuchangia katika kuboresha miundombinu ya shule hiyo.
Pia mdau wa maendeleo Mkurugenzi Mtendaji wa Glaring Future Foundation (GFF), Bi. Aisha Msantu, alisema katika uzinduzi huo amechangia madawati 60 na kutoa wito kwa wananchi kuchangia miundombinu ya shule ili Watoto waweze kupata elimu bora katika mazingira sahihi.
Naibu Waziri ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, kazi, vijana, Ajira na wenye ulemavu, Mhe. Anthony Mavunde, akiongea jambo na Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo kabla ya kuzindua shule shikizi ya Msingi Chiwondo iliyopo kata ya Nala jijini Dodoma.
Wanafunzi wa shule ya shikizi ya Msingi Chiwondo iliyopo kata ya Nala jijini Dodoma wakitoa burudani kwa mgeni rasmi Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo kabla ya kuzindua shule hiyo jana.
Viongozi wa meza kuu wakisikiliza hotuba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Glaring Future Foundation(GFF), Bi. Aisha Msantu wakati wa uzinduzi shule ya shikizi ya msingi Chiwondo iliyopo kata ya Nala jijini Dodoma
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi, akizungumza kabla ya mgeni rasmi Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo kuzindua shule shikizi ya Msingi Chiwondo iliyopo kata ya Nala jijini Dodoma.
Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Prof David Mwamfupe akizungumza kabla ya uzinduzi wa shule shikizi ya Msingi Chiwondo.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini naye alipata nafasi ya kuzungumza na wananchi wa Nala wakati wa uzinduzi wa Shule shikizi ya msingi ya Chiwondo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge akizungumza kwenye uzinduzi wa Shule shikizi ya Msingi Chiwondo.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini Mhe. Anthony Mavunde akizungumza na wapigakura wa Jimbo lake juu ya utekelezaji wa ahadi alizozitoa wakati akiomba kura na mikakati yake kuhakikisha jimbo lake linapiga hatua mbele katika elimu.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule shikizi ya Msingi Chiwondo wakifuatilia hotuba ya Mbunge wao Mhe. Anthony Mavunde aliyefanikisha kuwaondolea adha ya kutembea mwendo wa kilometa 20 kufuata elimu kwenye shule ya mbali.
Mbunge wa Dodoma mjini Mhe. Anthony Mavunde akizungumza kwa msisitizo mbele ya mgeni rasmi Waziri wa OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo pamoja na wananchi wa Nala na wanafunzi (hawapo pichani) waliohudhuria uzinduzi wa Shule shikizi ya Msingi Chiwondo.
Waziri wa OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi wa uzinduzi wa Shule shikizi ya Msingi Chiwondo akizungumza na wananchi wa Nala (hawapo pichani) alipoongoza wananchi hao kwenye tukio muhimu la uzinduzi wa shule yao ambayo imesaidia wanafunzi kuacha kutembea mwendo mrefu kufuata elimu.
Baadhi ya wananchi na wadau wa elimu waliojitokeza kuhudhuria uzinduzi wa shule shikizi ya Msingi Chiwondo wakimsikiliza mgeni rasmi Mhe. Selemani Jafo ambaye ni Waziri OR-TAMISEMI.
Madarasa mapya ya shule shikizi ya msingi Chiwondo.
Waziri wa OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo akikata utepe kuashiria uzinduzi wa shule ya msingi Chiwondo.
Uzinduzi rasmi wa shule shikizi ya msingi Chiwondo na Mhe. Selemani Jafo ambaye ni Waziri OR-TAMISEMI.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.