Shule 10 za elimu ya msingi za serikali na binafsi jijini Dodoma zimenufaika baada ya kupatiwa Vishikwambi 700 ambavyo vitawawezesha wanafunzi wa Jiji la Dodoma kusoma na kujifunza ki-eletroniki kufuatia utekekezaji wa mradi wa ugawaji wa vishikwambi kupitia Shirika la PROFUTURO pamoja na DON BOSCO.
Akimuwakilisha Mgeni Rasmi Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mhe. Patrobas Katambi amempongeza Mbunge Anthony Mavunde kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo katika kutatua changamoto za Elimu, na kuwataka wanafunzi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma kusoma kwa bidii ili kuunga mkono juhudi za mbunge wao Mhe. Anthony Mavunde. Aidha, amezitaka shule zilizopata vishikwambi hivyo kuvitunza na kuvitumia kuchochea ufaulu kwa wanafunzi wao.
Katambi amesema kuwa wanafunzi wanatakiwa kusoma kwa bidii ili kujikwamua kielim. "Ndugu zangu wanafunzi, msichezee elimu mnayoipata kwa sababu ndiyo urithi wetu wa maana ya kipekee hapa duniani. Msiwekeze kwenye anasa na mapenzi muwapo shuleni" alisisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.
"Tangu nimekuja Dodoma kama Mkuu wa Wilaya, nimejifunza jambo kubwa kupitia wewe la kuwapenda wananchi wako sana na kuweka msisitizo mkubwa kwenye Elimu kama silaha ya kuwakomboa wanafunzi katika Jimbo lako. Hongera sana Mheshimiwa Mavunde kwa kuendelea kuboresha sekta ya Elimu ukishirikiana na wadau kama hawa PROFUTURO, Dodoma Jiji lazima iwe tofauti na majiji mengine kiteknolojia na wewe haya unayajibu kwa vitendo" Alisema Katambi.
Aliendelea kusema "kazi unayoifanya ni kubwa na yenye tija kwa wana Dodoma na Taifa kwa ujumla. Mimi ni mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini, ni sehemu ya ushuhuda wa uchapa kazi wa Mbunge Anthony Mavunde. Kwa kweli ni mbunge wa mfano, mwenye uongozi shirikishi na ninaridhika na kazi anayofanya mbunge wetu" alifafanua zaidi.
Kabla ya hapo wakati akimkaribisha mgeni rasmi, Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe. Anthony Peter Mavunde amelishukuru shirika la PROFUTURO kwa kuchangia maendeleo kwenye sekta ya Elimu Jimboni Dodoma kuunga mkono juhudi na mkakati wa kuigeuza Dodoma Jiji kama moja ya maeneo yenye matumizi makubwa ya Sayansi na Teknolojia ambapo wanafunzi watajifunza masomo yao ya kawaida ya kwenye mtaala ki-eletroniki.
Awali akitoa maelezo ya mradi, Mwakilishi wa Shirika la PROFUTURO na Don Bosco Net Padri Peter Mutechura ameelezea namna ambavyo Shirika hilo limejikita kutoa huduma katika kuboresha sekta ya elimu kupitia Teknolojia na kuahidi kuendelea kushirikiana na Mbunge Mavunde kutatua changamoto mbalimbali za Elimu katika Jimbo la Dodoma Mjini.
Shule za msingi 10 zilizopewa vishikambi ni shule za msingi za Mlimwa, Mbwanga, Ihumwa, Chigongwe na Mazengo. Nyingine ni Brother Martin, Misericodia, Maria De Mattias, Chemchem na Capital.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.