MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini Mhe. Anthony Mavunde ameitaka TANESCO pamoja na Mkandarasi wa Mradi wa Ujazilizi (Densification) Kampuni ya Derm Electrics kuongeza kasi ya usambazaji wa huduma ya nishati ya umeme ili kuyafikia maeneo mengi Zaidi ambayo bado hayaunganishwa na umeme Jijini Dodoma.
Mbunge Mavunde ameyasema hayo leo katika ukumbi wa Jiji la Dodoma wakati wa kikao baina ya TANESCO, Kampuni ya Derm Electrocs na Madiwani wa Jiji la Dodoma ambao maeneo yao yanaguswa na mradi wa Ujazilizi wa Umeme pamoja na mradi mwingine wa PERI URBAN.
Akitoa maelezo ya awali Meneja wa TANESCO Kanda ya Kati Ndugu Frank Chambua amewahakikishia viongozi juu ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa Ujazilizi wa Umeme na kwamba watamsimamia mkandarasi kufanya kazi ndani ya muda wake wa mkataba na ukiwezekana kazi kumalizika kabla ya muda wa mkataba wa mwaka mmoja ili wananchi wa Dodoma waanze kunufaika na huduma hiyo ya Nishati ya umeme kwa lengo la kuchochea maendeleo katika maeneo husika.
“Katika Kata 41 za Jimbo la Dodoma yapo baadhi ya maeneo ambayo bado hayajaunganishwa na nishati ya umeme, naishukuru Serikali kwa kututengea zaidi ya shilingi bilioni 100 kutekeleza miradi ya umeme mkoani Dodoma, ambao ikikamilika itaiwasha Dodoma yote na hivyo kuchochea maendeleo na ajira katika maeneo husika.
Pamoja na kazi nzuri anayofanya Mkandarasi Derm Electronics kuyafikia maeneo mengi ndani ya muda mfupi, ninawataka muongeze kasi zaidi ili wananchi wanufaike mapema na huduma hii ya nishati jambo ambalo naamini lipo ndani ya uwezo wetu” amesema Mavunde.
Akitoa neno la shukrani, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Prof. Davis Mwamfupe amempongeza Mbunge Mavunde kwa namna ambavyo analisimamia suala la utekelezaji wa miradi ya umeme na kuwataka Madiwani kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi na TANESCO wakati wa utekelezaji wa miradi hii ambayo italeta mageuzi makubwa katika Jiji la Dodoma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.