Na. Dennis Gondwe, DODOMA
TIMU ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma inayoshiriki mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa shule za Sekondari (UMISSETA) imepewa zawadi ya ‘tracksuit’ 100 na kutakiwa kulinda heshima ya jiji hilo kwenye mashindano hayo.
Zawadi hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde katika hafla fupi ya kuwakabidhi ‘tracksuit’ hizo iliyofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Dodoma leo mchana.
Mbunge Mavunde amesema kuwa timu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma inayoshiriki mashindano ya UMISSETA ihakikishe inalinda heshima ya jiji hilo kwa kufanya vizuri katika michezo hiyo. “Leo nimekuja kuwapatia zawadi ya “tracksuit” 100 kwa ajili ya kuleta hamasa kwenu. Nitaendelea kutoa “tracksuit” nyingine mpya kila mwaka. Nitahakikisha ninawasimamia vizuri, nahitaji kuona vipaji vinakuwa na kulindwa. Michezo inaajiri watu wengi. Wananchichezo wengi wanapata mishahara mikubwa kuliko mawaziri na wakurugenzi” amesema Mbunge Mavunde.
Awali, Mkuu wa Idara ya Elimu Sekondari, Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Upendo Rwenyemamu alimtaarifu mbunge huyo kuwa timu ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma inayoshiriki mashindano ya UMISSETA ngazi ya wilaya inaendelea na mazoezi. Amesema kuwa timu hiyo inatarajia kuchuana na timu za wilaya nyingine ili kuunda timu itakayouwakilisha Mkoa wa Dodoma katika michezo ya UMISSETA ngazi ya Taifa.
Aidha, alimpongeza mbunge huyo kwa utayari wake katika kuendeleza sekta ya elimu jijini hapo. “Mheshimiwa Mbunge tunayofuraha kuwa nawe hapa. Tunakushukuru kwa utayari wako wa kutuunga mkono si katika michezo pekee, bali katika elimu kwa ujumla. Mchango wako ni mkubwa katika kukuza taaluma Jiji la Dodoma” amesema Mwalimu Rweyemamu.
Kwa upande wake mshiriki wa michezo ya UMISSETA jiji la Dodoma, Rehema Zahoro amesema kuwa matarajio ya timu yao ni kuleta makombe mengi.
Michezo ya UMITASHUMTA na UMISSETA mwaka 2021 inaongozwa na kaulimbiu isemayo “Michezo, Sanaa na taaluma kwa maendeleo ya viwanda”.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.