MBUNGE Jimbo la Dodoma Mjini, Mhe. Anthony Mavunde amekabidhi matofali 5,000 yenye thamani ya shilingi milioni nane kwa uongozi wa Kata ya Mpunguzi Jijini Dodoma sambamba na saruji mifuko 100 kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa shule mpya ya Sekondari ya Nkulabi.
Hafla ya kukabidhi imefanyika katika Kijiji cha Nkulabi Oktoba 5, 2021 na kuhudhuriwa na Naibu Meya wa Jiji la Dodoma Emmanuel Chibago ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matumbulu na wananchi wa Kata ya Mpunguzi.
“Nawapongeza sana wananchi wa Nkulabi kwa moyo wenu wa kujitolea mpaka tumefikisha wote hapa ujenzi wa shule hii” alisema Mavunde akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo.
Mbunge huyo pia aliishukuru Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutenga shilingi milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.
“Tunaishukuru pia Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutenga fedha shilingi milioni 40 kwa ajili ya kukamilisha madarasa haya matatu ambayo tumeyaanza” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Naibu Meya Chibago alimshukuru Mbunge huyo kwa kazi kubwa anayofanya ya kuwahudumia wananchi na kuwahakikishia kwamba Jiji la Dodoma litaendelea kutenga fedha kuboresha miundombinu ya Elimu na kuunga mkono juhudi za wadau kama Mbunge Mavunde pamoja na wananchi.
Naye diwani wa Kata ya Mpunguzi Mhe. Innocent Nyambuya alimshukuru mbunge Mavunde kwa namna anavyoshirikiana nao kutatua changamoto mbalimbali za kwenye sekta ya Elimu na kuahidi kuwa naye bega kwa bega katika kuwaletea maendeleo wananchi wa kata hiyo.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.