Na. Faraja Mbise, DODOMA
MBUNGE wa Jimbo la Dodoma mjini Anthony Mavunde, ameahidi kuwatengenezea mazingira mazuri na rafiki ya kufanyia biashara mama lishe waliopo pembezoni mwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Mavunde alizungumza hayo mara baada ya kumaliza zoezi la uzinduzi wa ujenzi wa jengo la kupumzikia wananchi lilipo nje ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Aidha, Mavunde aliahidi kuwaboreshea na kuwatengenezea mazingira rafiki ya kufanya biashara ya chakula na kukarabati miundombinu kama vile kuwatengenezea meza na viti za kufanyia biashara pamoja na kuweka maeneo nadhifu.
Mavunde alisema “sambamba na hilo nafahamu ya kwamba, asilimia kubwa ya wanaokaa pale hawavimudu vyakula ambavyo watu wengi hapa tunavimudu vyakula vya mahotelini...”.
Hata hivyo, Mavunde aligusia wananchi wa kipato cha chini wasioweza kumudu gharama kubwa za kununua chakula kwa ajili ya wagonjwa wao hivyo kuahidi kuwasaidia mama lishe kuboresha maeneo yao ya kufanyia kazi kuwa safi na salama ili waweze kutoa huduma nzuri ya chakula kwa wananchi.
Kwa upande wa mama lishe nao hawakuwa nyuma walipongeza juhudi zinazofanywa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, hususani katika uzinduzi wa ujenzi wa jengo la kupumzikia wananchi uliofanyika leo hii jijini Dodoma.
Mama lishe, Pili Elius katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na mkazi wa Chinyoya alisema “tunamshukuru mbunge wetu kwa alichotufanyia, sisi kama mama lishe tunamuomba Mungu ampe maisha marefu na hili jengo linalojengwa litaleta manufaa kwa wanaouguza wagonjwa wao. Miaka mingi sana wanalala hapo nje, mvua zinawanyeshea na baridi, tunaona ni jambo jema sana kuhusu ujenzi huu”.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini alitoa ahadi hiyo alipokuwa akiongea na mamia ya wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa ujenzi wa jengo la kupumzikia wananchi wanaoenda kuona wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kutokana na changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa mahali pa kupumzikia.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.