UJUMBE wa watu nane kutoka Jiji la Linz nchini Austria ukiongozwa na Meya wa Jiji hilo Klaus Luger na Naibu Meya Detlef Wimmer umewasili Jijini Dodoma jana Februari 12, 2018, kwa ziara ya siku mbili ambapo pamoja na mambo mengine wataikabidhi Halmashauri ya Jiji la Dodoma gari moja la zimamoto.
Meya Luger na ujumbe wake wakiwemo Maofisa wanne wa idara ya Zimamoto walipokelewa na mwenyeji wao Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Mhe. Prof. Davis Mwamfupe kwa pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji ikiongozwa na Godwin Kunambi.
Akizungumzia ujio viongozi hao, Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma Mhe. Prof. Davis Mwamfupe alisema kuwa ziara hiyo ya Mstahiki Meya wa Jiji la Linz inalenga kuendeleza ushirikiano baina ya Jiji lake na jiji la Linz la nchini Austria.
Baada ya kupokelewa, ugeni huo ulitembelea maeneo kadhaa ya Jiji la Dodoma, ikiwemo shamba na kiwanda cha kusindika Zabibu cha kikundi cha akina Mama kilichopo Kata ya Mpunguzi, Shule ya Msingi Mpunguzi, pamoja na Dampo la kisasa linalohifadhi taka kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kuzika ardhini (Sanitary Landfill) lililopo eneo la Chidaya katika Kata ya Matumbulu.
Ziara ya Meya huyo na msafara wake itahitimishwa Februari 13, 2018, ambapo wanatarajia kusaini hati ya makubaliano ya mashirikiano katika nyanja kadhaa za Kiuchumi na Kijamii.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.