Na Shaban Ally, DODOMA
MSTAHIKI MEYA wa Jiji la Dodoma, Prof. Davis Mwamfupe amewapigia chapuo madiwani kuongezewa posho kama ilivyofanywa kwa watumishi wa umma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ameyasema hayo alipohudhuria hafla fupi ya kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha maslahi ya watumishi wa umma na kwa kuimarisha miundombinu, hafla iliyoandaliwa na Mkuu wa mkoa wa Dodoma na kufanyika katika ukumbi wa PSSSF jijini hapa.
"Kuna aina fulani ya posho yenyewe inahesabika katika pensheni, inahesabika katika mikopo ni posho ya sisi madiwani. Kwahiyo, naamini utakapokuwa (RC) unatoa mrejesho kwa Rais utasema miongoni mwa viongozi ambao tunao kisiasa wapo wengine ambao posho yao inahesabika katika mikopo" alisema, Prof. Mwamfupe.
Mstahiki Meya huyo aliwaasa watumishi wa umma katika Jiji la Dodoma kuwapa huduma iliyotukuka wananchi kutoka maeneo tofauti ya nchi watakao kuwa wanahitaji huduma katika jiji hilo. Alisema, kwa kuwa hafla hiyo ilikuwa mubashara katika vyombo vya habari, wananchi kutoka kila pande ya Tanzania waliweza kuona jinsi watumishi hao wa umma wanavyo mpongeza Rais kwa ongezeko la asilimia 23.3 la mishahara na posho.
Aidha, alimalizia kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa mengi mazuri anayoendelea kuyafanya katika kuboresha maisha ya wananchi wake.
Hafla ya kumshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na kuhudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya, Meya wa Jiji la Dodoma, wakuu wa taasisi za Serikali na watumishi wa umma.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.