MBUNGE wa Jimbo la Dodoma mjini, Anthony Mavunde, amekabidhi madawati 590 kwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma ili kuchangia mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi na kuongeza ufaulu.
Mbunge Mavunde, amesema kuwa ametumia shilingi Milioni 70 kutoka kwenye Mfuko wa Maendeleo wa Jimbo katika kuhakikisha anafikia malengo hayo ya kutatua changamoto ya madawati kwenye shule za msingi, na kwamba katika halmashauri hiyo, shule 32 zilitoa taarifa juu ya upungufu wa madawati na shule tisa hazikutoa taarifa, hivyo inafanya shule zilizopatiwa madawati hayo kuwa 41.
“Na sisi tuna muunga mkono Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo ambayo aliyatoa katika Ofisi ya TAMISEMI kuhakikisha kwamba hakuna mtoto ambae anakaa chini. Sisi Dodoma tumelianza hili kupitia Mfuko wa Jimbo na Halmashauri ya Jiji la Dodoma“ amesema Mbunge Mavunde.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Mwalimu Joseph Mabeyo ameishukuru Serikali na uongozi uliopo chini ya Mbunge na kuomba mpango wa kutatua changamoto ya madawati katika shule za Halmashauri hiyo uwe endelevu katika kuhakikisha shule zilizobaki au kukosa madawati zinafikiwa na kupatiwa suluhu katika muda sahihi. Suluhu hiyo itawawezesha wanafunzi kupata mazingira sahihi ya kujifunzia, ameongeza.
“Nichukue nafasi hii kumshukuru Mbunge, kwa maamuzi yake makubwa ambayo ameyafanya kwa kutumia fedha za jimbo ambazo ni takribani milioni 70 kwa ajili ya utengenezaji wa madawati kwa shule za msingi“ amesema Mwalimu Mabeyo.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii katika Halmashauri hiyo, Sospeter Mazengo amekiri kuwa halmashauri hiyo ina changamoto ya madawati na kupitia maono ya Mbunge itakuwa rahsi kutatua changamoto hiyo.
Picha za matukio mbalimbali wakati wa makabidhiano
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.