MFUMO wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato ya Kodi, Maduhuli, Tozo na Huduma (Government electronic Payment Gateway - GePG) umeongeza makusanyo ya maduhuli serikalini kwa asilimia 292 kutoka Sh bilioni 688.7 katika mwaka 2015/16 hadi Sh trilioni 2.699 mwaka 2019/2020.
GEPG pia imeboresha makusanyo katika taasisi 668 zilizojiunga likiwemo Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambalo ukubwa wake umeongezeka kwa asilimia 40 kutoka Sh trilioni 3.2 mwaka 2018 hadi Sh trilioni 4.8.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James (pichani) aliyasema hayo baada ya kupokea ripoti ya tathmini ya mfumo wa kieletroniki wa ukusanyaji mapato na usimamizi wa fedha, iliyoandaliwa na watalaamu wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM).
James alisema GePG ni miongoni mwa mifumo minne mikubwa, ambayo imebuniwa na kutengenezwa na wazawa na kusimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango.
Mfumo mwingine ni wa Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi na Malipo ya Serikali (MUSE), Mfumo wa Usimamizi wa Miradi ya Maendeleo (NPMIS) na Mfumo wa Usimamizi wa Misamaha ya Kodi.
Katibu Mkuu huyo alisema matumizi ya mifumo hiyo, yameleta mageuzi makubwa serikalini. Alitaka kila mtu anayelipa huduma ya umma, lazima apewe control namba na taasisi inayotoa huduma.
Pia alisema kila taasisi inayotaka kutekeleza mradi wowote wa maendeleo, lazima ihakikishe inatumia mfumo katika kufanya maombi ya kutekeleza mradi.
"Nasisitiza kwamba maafisa masuhuli wote kuhakikisha mnapata ridhaa ya Wizara ya Fedha na Mipango kabla ya kufanya ununuzi, uandaaji, usimikaji na matumizi ya mfumo wowote wa kielektoniki katika maeneo yenu," alisema James.
Akiwasilisha ripoti ya Tathmini ya Mfumo wa GePG, Mhadhiri Mwandamizi UDSM, Profesa Joel Mtebe alisema katika utafiti waliofanya kwa taasisi 271 katika kanda saba kwenye mikoa 11 kwa watendaji 384 na wakuu wa taasisi 257, asilimia 87 mfumo huo umesaidia kuongeza makusanyo ya maduhuli serikalini.
Profesa Mtebe alisema katika utafiti huo, asilimia 77 ya watumiaji wa mfumo huo wamesema ni bora na umesaidia kuongeza malipo ya serikali na asilimia 87 kati yao wamesema una ubora na asilimia 82 wamesema mfumo huo umeongeza uwezo wa serikali kukusanya maduhuli.
Katibu Mkuu alisema GePG ilianza kutumika Julai Mosi mwaka 2017 ili kukabiliana na changamoto serikalini zikiwemo za ukusanyaji fedha za umma, gharama kubwa za miamala iliyohusika makusanyo hayo, utararibu usio rafiki kwa mlipaji wa huduma na machaguo machache ya njia ya kulipia huduma.
Alisema mfumo huo umeleta faida 12 ikiwemo ya kuongeza uwazi na udhibiti makusanyo, upatikanaji wa taarifa sahihi za makusanyo na kwa wakati na pia kuchochea ubunifu katika ukusanyaji fedha na kutoa huduma bora na rahisi ya malipo.
"Fedha kufika haraka kwenye akaunti za makusanyo zilizopo Benki Kuu (BoT), kusaidia benki na mitandao ya simu kuwa na sehemu moja ya kuunganisha mifumo yao, kuwezesha benki na mitandao kuwa na mazingira rafiki na ya usawa katika uusanyaji fedha,”alisema Katibu Mkuu Hazina.
Pia kuzisaidia taasisi za umma kupunguza gharama zinazotokana na uwekezaji katika miundombinu ya Tehama, urahisi katika usuluhishi wa mialama na usuluhishi wa taarifa za kibenki, kupunguza gharama za miamala inayohusu ukusanyaji na kumuongezea mlipaji wa huduma machaguo mengi ya njia ya kulipia huduma za umma kama benki, wakala na mitandao ya simu.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio alisema shirika hilo tangu limejiunga na GePG Aprili 2019, makusanyo ya kila mwezi yamepanda kutoka takribani Sh milioni 60 kwa mwezi hadi Sh milioni 100.
Erio alisema GePG imeleta mabadliko makubwa kwa shirika hilo katika ukusanyaji wa michango kutoka kwa wanachama wa sekta rasmi na isiyo rasmi na kwenye kodi ya pango katika vitega uchumi.
Tangu kujiunga na mfumo huo, NSSF imepunguza idadi ya akaunti ambazo zilikuwa zikitumika kutoka 78 hadi tatu, hivyo imekuwa rahisi kuweka hesabu sawa.
Mhasibu Mkuu wa Serikali, Francis Mwakapalila alisema kuanzishwa kwa Mfumo wa Usimamizi na Udhibiti wa Matumizi na Malipo ya Serikali (MUSE), kumepunguza gharama ambazo serikali ilikuwa ikitumia kulipia mifumo kutoka nje.
Mwakapalila alisema serikali kwa kutumia mfumo wa EPICA ilikuwa ikitumia Sh bilioni 5.6 kwa ajili ya kununua leseni na Sh bilioni 1.5 zilitumika kulipia uanachama na Sh milioni 500 kwa ajili ya kusaidia kuangalia mifumo hiyo inavyofanya kazi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.