Na. Getruda Shomi, DODOMA.
WAHUDUMU wa Kituo cha Afya Mkonze wameanza kupatiwa mafunzo ya mfumo wa kielektroniki wa huduma za afya (Government of Tanzania Health Management Information System - GoTHOMIS) utakaorahisisha kutunza kumbukumbu za wagonjwa na taarifa za malipo, utarahisisha kupatikana kwa historia ya mgonjwa na utoaji wa huduma kirahisi.
Mafunzo hayo yanatolewa na Afisa TEHAMA katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Caesar Faustine (pichani juu aliyesimama). Caesar alikuwa akitoa maelekezo ya namna ya kutumia mfumo huo wa kielektroniki kusajili wagonjwa, vipimo na namna ya ulipaji wa bili za matibabu.
Afisa TEHAMA huyo alisema “Serikali imeamua kuunda mfumo huu ili kuweza kurahisisha kazi kutoka kwenye kutumia mafaili hadi kwenye mifumo ya kielektroniki ambapo itasaidia kutunza kumbukumbu za wagonjwa na wagonjwa watapewa namba zao za kwenye mifumo ili wanapotaka tena kupata matibabu waweze kupatiwa kulingana na kumbukumbu za matibabu ya awali” alisema Faustine.
Wahudumu wa vituo vya afya watatumia mfumo huo kwa kutumia kompyuta ambazo zitawekwa kwenye kila kitengo cha matibabu kama vile mapokezi, maabara, maduka ya dawa, X-ray, na kadharika. Aidha, mfumo huo unauwezo wa kuchapa risiti za malipo.
Akizungumzia mfumo huo Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkonze, Dkt. Leticia Siwalima aliahidi kuwa watautumia vizuri kama walivyoelekezwa kwa sababu unalengo la kurahisisha kazi na kutunza kumbukumbu za wagonjwa.
“Mfumo huo ni mzuri na utasaidia kutunza kumbukumbu za wagonjwa, hivyo mpaka mwisho wa semina hii tutakuwa tumeweza kuutumia” alisema Dkt. Siwalima.
Naye Afisa TEHAMA John Longino alisema kuwa mafunzo na mazoezi ya utumiaji wa mfumo huo yanaendelea vizuri na wanamatumaini makubwa kuwa baada ya kukamilika kwa mafunzo na mazoezi, mfumo utaanza kutumia rasmi kuendesha shughuli za kila siku za utoaji huduma za afya kituoni hapo.
Hata hivyo, hadi sasa kituo kila kompyuta tano tu zilizounganishwa kwenye mfumo, wakati mahitaji halisi ni kompyuta 12. Tayari kituo kimeanza kuangalia namna ya kupata kompyuta zinazohitajika ambapo Kaimu Mganga Mfawidhi ameomba wadau kujitokeza ili kuchangia upatikanaji wa vifaa hivyo.
Ikumbukwe kuwa Mwenge wa Uhuru wa mwaka huu umebeba kauli mbiu isemayo ‘TEHAMA ni msingi wa Taifa endelevu, itumike kwa usahihi na uwajibikaji”. Hivyo basi, Jiji la Dodoma limejiwekea mikakati kuhakikisha kila kituo cha Afya na Zahanati inatumia mfumo wa kielektroniki ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.