BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dodoma, limemchagua Emmanuel Chibago kuwa Naibu Meya baada ya kumshinda Said Kitegile katika uchaguzi uliofanyika mapema wiki hii.
Akitangaza matokeo hayo katika mkutano wa mwaka wa Baraza la Madiwani, msimamizi wa uchaguzi huo, Godwin Kunambi alisema kuwa Emmanuel Chibago (CCM) ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matumbulu alipata kura 52 kati ya kura 57 zilizopigwa. Mpinzani wake Said Kitegile (CHADEMA) ambaye ni Diwani wa Kata ya Madukani alipata kura 5 kati ya kura 57 zilizopigwa.
Akitoa shukrani zake kwa wajumbe, Naibu Meya Chibago alisema kuwa atakapokwenda kinyume yupo tayari kukosolewa. “Shukrani kwa imani mliyonipa na kura mlizonipigia. Naomba ushirikiano wenu” alisema Chibago. Mhe. Chibago alimuomba Mhe. Jumanne Ngede kuwa tayari kumpa ushirikiano kutokana na uzoefu wake katika nafasi hiyo ambayo ameitumikia kwa vipindi vinne (miaka 4) tangu kumalizika kwa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika mwaka 2015.
Kwa upande wake, Said Kitegile alisema kuwa ameyapokea matokeo hayo na kumpongeza kwa dhati Diwani Mheshimiwa Chibago.
Katika nafasi za wenyeviti wa kamati, Mhe. David Bochela, Diwani wa Kata ya Mkonze kwa mara nyingine alichaguliwa tena kuwa mwenyekiti wa kamati ya Mipango Miji na Mazingira kwa kupata kura 16. Kamati ya Uchumi, Elimu na Afya, mwenyekiti alichaguliwa Mhe. Daud Mkhandi ambaye ni Diwani wa Kata ya Nkuhungu kwa kupata kura 17.
Naye Naibu Meya aliyemaliza muda wake Mheshimiwa Jumanne Ngede aliwashukuru wajumbe wa Baraza kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote alichotumikia kama Naibu Meya wa Jiji. Aidha, alimpongea Naibu Meya mpya Mhe. Emmanuel Chibago na kumuahidi ushirikiano wakati wote.
Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi alisema kuwa yaliyopita yamepita, mtazamo uwe kutoa huduma kwa wananchi. “Kamati hizi zinaenda kuwa na sura mpya ili kuwa na lengo la pamoja. Tafuteni kwanza ufalme wa mbingu na mengine mtazidishiwa. Kwentu Dodoma 'ufalme wa Mungu' ni kutoa huduma bora kwa wananchi” alisema Kunambi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.