MAMLAKA za serikali za mitaa katika mikoa ya Dodoma na Singida zimetakiwa kuhakikisha mabanda yao yanakuwa ‘live’ katika uwanja wa maonesho wa Nanenane kwa kipindi cha mwaka mzima ili kutoa fursa kwa wananchi kujifunza na kuziongezea Halmashauri zao mapato.
Agizo hilo lilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Seleman Jafo alipokuwa akifungua rasmi maonesho ya Nanenane jijini Dodoma siku ya Jumanne 05 Agosti, 2019 katika viwanja vya Nanenane vilivyopo Nzuguni Jijini Dodoma.
Waziri Jafo alisema “nataka uwanja wa maonesho ya Nanenane uwe endelevu, usiwe uwanja mfu. Halmashauri zote hakikisheni mabanda ya Halmashauri yanakuwa ‘live’ mwaka mzima”. Kila Halmashauri imepata heka mbili, na kuzitaka kutengeneza miundombinu kwa ajili ya umwagiliaji wa njia ya matone. “Wekeni hapa ‘drip irrigation’. Maana hapa mwaka mzima mboga zitakuwa zinalimwa Nanenane. Na mabwana shamba wanapangiwa hapa kama kituo cha kazi. Hilo nahitaji litekelezwe. Mwakani kila Halmashauri itakuwa na bustani nzuri. Vilevile, ni chanzo cha mapato” alisema Waziri Jafo.
Akiongelea kilimo na ufugaji wenye tija, waziri huyo aliwataka wadau wa kilimo na mifugo kutumia fursa za tafiti zinazofanyika nchini katika maeneo hayo. Alisema kuwa tafiti hizo zinalenga kuongeza tija katika mazao ya kilimo na mifugo.
Kuhusu uendelezaji wa bidhaa za ngozi, alisema kuwa sekta hiyo inapiga hatua. “Wakati wa kutembelea mabanda nimekuta viatu vya ngozi. Hakikisheni vijana wanavaa viatu vinavyozalishwa mikoa ya Dodoma na Singida” alisema waziri Jafo. Aidha, aliwashauri wananchi kujenga utamaduni wa kununua bidhaa zinazozalishwa nchini kwa lengo la kujenga soko la ndani.
Katika salamu za Mkuu wa Mkoa wa Singida, Canon Dkt. Rehema Nchimbi alisema kuwa Mkoa wake unafanya vizuri katika sekta ya kilimo na mifugo kutokana na uwepo wa maonesho ya Nanenane.
“Nanenane ipo pia Singida kama ilivyo Dodoma kwa tafsiri ya kuleta mabadiliko kwa wananchi wetu. Nanenane imetusaidia sana Singida. Imeifanya Singida isiwe kame, masikini na ya njaa. Tumezalisha ziada ya chakula kwa miaka mitano iliyopita. Singida tunachakula cha kutosha na hatuna njaa. Singida hatuzalishi mazao yanayostahimili ukame bali yanayotumia maji kwa ufanisi” alisema Dkt Nchimbi.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt Binilith Mahenge alisema kuwa Rais amejenga vituo vya afya nchi nzima na kuongeza bajeti ya dawa ili wananchi wanufaike na huduma za afya. “Mheshimiwa Waziri hakuna upungufu wa dawa. Lazima kila mwananchi awe na kadi ya bima ya afya CHF iliyoboreshwa kwa shilingi 30,000 kwa kaya na inahudumia watu sita 6” alisema Dkt Mahenge. Zaidi ya hapo utalazimika kulipa gharama ili unufaike na huduma ya afya kama hutakuwa na kadi hiyo, aliongeza.
Maonesho ya 26 ya Nanenane Nzuguni Dodoma yameshirikisha makampuni 36, wajasiriamali 300 na taasisi 43.
Waziri wa OR-TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo akipata maelezo kutoka kwa mmoja wa wajasirimali wanaoonesha bidhaa zao kwenye maonesho wa Nanenane Nzuguni alipotembelea mabanda yanayoonesha bidhaa mbalimbali. Wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Canon Dkt. Rehema Nchimbi.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.