NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Deogratius Ndejembi alisema kuna ulazima wa kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa shule ili kukidhi mahitaji yanayotokana na ongezeko la wanafunzi ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu.
Ndejembi alitoa wito huo akiwa mkoani Dar es Salaam, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya elimu inayojengwa kupitia mradi wa BOOST na SEQUIP katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.
Ndejembi alisema maeneo hayo yakitengwa, kuna ulazima wa kujenga shule za ghorofa badala ya majengo ya chini ili kutatua changamoto ya kukosa viwanja vya michezo vya watoto ambavyo ni muhimu kwa ajili ya kujenga afya ya akili.
“Michezo ni muhimu kwa ajili ya afya ya akili na makuzi ya watoto hivyo ni lazima kuwepo na ushirikiano wa viongozi kuanzia ngazi ya mtaa, kata, halmashauri, wilaya na mkoa katika kuhakikisha shule zinajengwa kwenda juu ili kupata maeneo ya viwanja vya michezo,” Ndejembi alisisitiza.
Aliongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kutafuta fedha kwaajili ya kuboresha elimu ya msingi na sekondari, hivyo ni lazima kuendelea kutenga maeneo ya ujenzi na kuyatumia vizuri ili yawe na tija.
Aidha, Ndejembi aliipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa kukamilisha ujenzi wa shule mpya na ukarabati wa miundombinu ya elimu, kupitia fedha za mradi wa BOOST na SEQUIP zilizopatikana kutokana na jitihada za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kuendelea kuboresha miundombimu ya elimu nchini.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za ujenzi wa miundombinu ya elimu kupitia mradi ya BOOST na SEQUIP na kuahidi kuendelea kusimamia vizuri matumizi ya fedha hizo ili ziwe manufaa kwa taifa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.