Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli leo tarehe 14 Marchi, 2018 ameweka jiwe la msingi la kipande cha pili cha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) kinachoanzia Morogoro hadi Makutupora Mkoani Dodoma.
Sherehe za uwekaji jiwe la msingi katika mradi huo zimefanyika katika Kijiji cha Ihumwa nje kidogo ya Mji wa Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Tulia Ackson, Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama, Mabalozi wa Uturuki na Uingereza hapa nchini, Wabunge, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Dodoma Profesa Davis Mwamfupe, Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma Bw. Godwin Kunambi na wananchi wa Dodoma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Bw. Masanja Kadogosa amesema ujenzi wa kipande cha pili cha reli chenye urefu wa kilometa 422 utagharimu Shilingi Trilioni 4.3 na ni sehemu ya mradi mkubwa wa ujenzi wa reli ya kati wa kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilometa 1,219.
Bw. Kadogosa amesema ujenzi wa kipande cha pili utakaofanyika kwa miezi 36 utakamilika ifikapo tarehe 25 Februari, 2021 na umetanguliwa na ujenzi wa kipande cha kwanza cha kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro utakaokamilika Novemba 2019.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema wakati wa ujenzi wa kipande cha pili che reli ya kati ukianza, ujenzi wa kipande cha kwanza umefikia asilimia 9 na kwamba treni zitakazotumia reli hiyo zitakuwa na uwezo wa kubeba tani 10,000 za mzigo kwa wakati mmoja (sawa na malori 500 ambayo yangesafirisha mizigo kwa barabara) na itakuwa na uwezo wa kwenda kasi ya kilometa 120 kwa saa wakati treni ya abiria itakuwa na uwezo wa kwenda kwa kasi ya kilometa 160 kwa saa.
Kabla ya kumkaribisha Mhe. Rais Magufuli, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amemshukuru kwa msukumo mkubwa aliouweka katika utekelezaji wa miradi na shughuli kubwa za Serikali ikiwemo ujenzi wa reli na amewataka watanzania kuunga mkono juhudi hizo.
Katika hotuba yake Mhe. Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa na utekelezaji wa mradi huo ambao amesema utasaidia kurahisisha na kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo na abiria, na pia utaokoa barabara ambazo zinaharibika kutokana na usafirishaji wa mizigo mizito kwa magari.
"Kwa kutumia reli hii mtu atasafiri kutoka Dar es Salaam hadi hapa Dodoma kwa saa 3 tu ikilinganishwa na saa 5 hadi 6 zinazotumika hivi sasa kwa gari, na pia mtu atasafiri kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza kwa saa 9 ikilinganishwa na saa 36 anazotumia sasa kwa kutumia treni" amesema Mhe. Rais Magufuli na kuongeza kuwa reli hiyo itakuwa na uwezo wa kusafirisha tani milioni 17 za mizigo kwa mwaka ikilinganishwa na ya sasa yenye uwezo wa kusafirisha tani milioni 5 tu.
"Bila shaka hii itaongeza mapato katika bandari yetu ya Dar es Salaam na pia kuimarisha biashara hususani kati ya nchi yetu na nchi za Burundi, DRC, Rwanda na Uganda" ameongeza Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais amewataka wananchi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa zinazotolewa na mradi huu mkubwa ambao utazalisha ajira za moja kwa moja 30,000 na zisizo za moja kwa moja 600,000 pamoja na miradi mingine ya ujenzi wa barabara, bomba la mafuta la kuanzia Hoima - Uganda hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania, mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji, ukarabati wa viwanja 11 vya ndege na ujenzi wa meli ya ziwa Victoria.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango kufuatilia utozaji wa kodi unaofanywa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ili kuepusha utozaji wa viwango ambavyo ni kero na amesisitiza kuwa "inatakiwa kulipa kodi isiwe kero, iwe ni heshima".
Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kulipa kodi ili fedha zinazopatikana ziendelee kugharamia miradi ya maendeleo ikiwemo kupeleka huduma muhimu za maji, elimu, afya na umeme ambapo Serikali imedhamiria ifikapo mwaka 2021 vijiji vyote nchini vipatiwe umeme.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.