RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni juzi tarehe 11 Aprili, 2021 wameshuhudia utiaji waini wa mikataba ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (East Africa Crude Oil Pipeline – EACOP) kati ya Serikali na kampuni za uwekezaji uliofanyika katika Ikulu ya Entebe nchini Uganda.
Hafla ya utiaji saini mikataba ya mradi huo ilihudhuriwa na Mawaziri na wawakilishi wa kampuni za uwekezaji ambazo ni Total ya nchini Ufaransa na CNOCC ya China.
Waheshimiwa Marais wameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa kwanza ambao ni wa uenyeji wa mradi kati ya Serikali ya Uganda na wawekezaji (Total na CNOCC), mkataba wa pili wa ubia ambapo Serikali ya Tanzania na Uganda zimetiliana saini na kampuni hizo (Total na CNOCC) na mkataba wa tatu wa masuala ya kikodi na usafirishaji ambapo Serikali ya Uganda imetiliana saini na kampuni hizo (Total na CNOCC).
Pamoja na kushuhudia utiaji saini wa mikataba hiyo, Waheshimiwa Marais pia walitia saini tamko la pamoja kuhusiana na utekelezaji wa mradi huo na wameagiza vipengele vilivyobaki katika utekelezaji wa mradi huo vikamilishwe haraka.
Mradi huo utahusisha ujenzi wa bomba la mafuta lenye kutumia teknolojia ya joto (heated oil pipeline) lenye urefu wa kilometa 1,445 ambapo kati yake kilometa 1,115 zinapita Tanzania. Uwekezaji katika mradi huu unatarakiwa kugharimu Dola za Kimarekani Bilioni 3.5, uzalishaji ajira takribani 10,000 wakati wa ujenzi na utasafirisha mapipa Bilioni 6.5 ya mafuta yaliyogundulika katika bonde la ziwa Albert nchini Uganda kwenda bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Rais Samia alimshukuru Mhe. Rais Museveni kwa kuahirisha hafla ya utiaji saini wa mikataba hiyo iliyopangwa kufanyika tarehe 22 Machi, 2021 ili kupisha maombolezo ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye wakati wa uhai wake alitoa mchango na msukumo mkubwa katika utekelezaji wa mradi huu mkubwa duniani.
Mhe. Rais Samia alisema mradi huu utakuwa na manufaa makubwa kwa nchi zote mbili kwa kuongeza mapato ya Taifa, kuzalisha ajira, kukuza utangamano na kuinua ustawi wa jamii.
Aidha, ametoa wito kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendeleza jitihada za kuimarisha miundombinu ya barabara, reli, bandari na viwanja vya ndege ili kuunga mkono uwekezaji huo pamoja na uwekezaji mwingine unaolenga kuimarisha uchumi na kuboresha maisha ya watu.
Mhe. Rais Samia amemhakikishia Mhe. Rais Museveni kuwa Serikali anayoingoza itaendeleza na kukuza zaidi ushirikiano na uhusiano wake na Uganda ikiwa ni pamoja na kuanzisha maeneo mapya ya ushirikiano.
Kwa upande wake Mhe. Rais Museveni alimshukuru Mhe. Rais Samia kwa kuitikia wito wake wa kuja kushuhudia utiaji saini wa mikataba hiyo na kufanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mhe. Rais Museveni alieleza sababu za kupitisha bomba hilo nchini Tanzania kuwa ni manufaa ya kiuchumi na pia kwa Uganda kutambua mchango wa Tanzania katika kumuondoa aliyekuwa Mtawala wa Uganda Nduli Idd Amin Dada na ushirikiano mwingine kama ndugu, jirani na rafiki wa kweli.
Aliongeza kuwa kwa kutekeleza mradi huo, Uganda pia itarahisisha mpango wake wa kununua gesi kutoka nchini Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suhulu Hassan akilakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uganda Mhe. Sam Kutesa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Entebe alipowasiri nchini Uganda kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suhulu Hassan akimtambulisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Liberata Mulamula kwa mwenyeji wake Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Museveni mara baada ya kuwasili katika Ikulu ya Entebbe Aprili 11, 2021 kwa ziara ya siku moja.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.