NAIBU Waziri wa Kilimo, Mhe. David silinde (Mb), ameshiriki katika Kongamano la Vijana na Wanawake kwenye Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa Nane Nane 2024 katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma .
“Wito wangu kwa vijana, wanawake na wananchi mliofanikiwa kuona bunifu, huduma, teknolojia mbalimbali zilizooneshwa katika maonesho haya mkatumie elimu na maarifa mliyoyapata kwa lengo la kujiletea mapinduzi halisi katika kuongeza tija, uzalishaji na ubora wa mazao yetu ya kilimo,” ameeleza Mhe. Silinde.
Pia Mhe. Silinde amesema Serikali ya Awamu ya Sita imefanya juhudi mbalimbali zenye malengo ya kuendeleza Sekta ya Kilimo ikiwa ni ni pamoja na kuongeza ajira kwa vijana kupitia Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (Building a Better Tommorow -BBT) ambayo inatekelezwa nchi nzima kwa lengo la kuwavutia vijana na kuwawezesha kupata ardhi yenye miundombinu ya umwagiliaji pamoja na mikopo ya riba nafuu na kuwaunganisha na masoko.
Kutokana na juhudi hizo Mhe. Silinde amesema Sekta ya Kilimo katika mwaka 2023 ilikua kwa asilimia 4.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 3.3 mwaka 2022. Vilevile, Sekta ya Kilimo imechangia asilimia 26.5 katika Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 26.2 mwaka 2022, imetoa ajira kwa wananchi kwa wastani wa asilimia 65.6 na kuchangia asilimia 65 ya malighafi za viwanda.
Vilevile Mhe. Silinde amebainisha kuwa Sekta ya Kilimo kwa upande wa mazao ilikua kwa asilimia 4.2 mwaka 2023 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 2.7 mwaka 2022; imechangia asilimia 16.1 kwenye Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 15 mwaka 2022; na imeendelea kuchangia asilimia 100 ya upatikanaji wa chakula.
Miradi mbalimbali imebuniwa kwa vijana ikiwemo uchimbaji wa visima, uwekaji wa miundombinu ya umwagiliaji, uwezeshaji wa mikopo nafuu yenye riba isiyozidi asilimia 4.5 kupitia Mfuko wa Pembejeo za Kilimo (Agricultural Input Trust Fund - AGITF) ambapo katika mwaka 2023/2024 mikopo yenye thamani ya Shilingi Milioni 950 imetolewa kwa vijana na wanawake; na kuhamasisha vijana kutoa huduma za ugani BBT Agricultural Extension kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.