Na. Dennis Gondwe, DODOMA
KATA ya Madukani jijini Dodoma imeadhimisha miaka 46 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ‘General Hospital’ na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wagonjwa na wanaowauguza kwa lengo la kuwahakikishia kuwa chama hicho kipo pamoja nao.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Madukani, Ezekiel Mwangosi aliyasema hayo alipoongoza viongozi wa kata hiyo kutembelea wagonjwa na kutoa misaada ya vitu mbalimbali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Mwangosi alisema “Kamati ya Siasa ya Kata ya Madukani tulikubaliana kuwa ni vema kuwatembelea wagonjwa na kutoa pole, kuwatakia afya njema na kuwapa zawadi ya vitu mbalimbali. Miongoni mwa vitu tulivyoleta leo ni mabeseni makubwa, chupa za chai, sabuni za unga, sabuni za miche na mafuta kwa kuvitaja vichache”.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa timu yake imefanikiwa kujionea utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM katika Kata ya Madukani na kuridhika. “Tumeshuhudia jengo kubwa la kina mama na majengo mengine yanakarabatiwa. Hivyo, hata tunapokuwa mtaani tuna mambo ya kujivunia kama wana CCM kwenye utekelezaji wa Ilani. Tunashukuru kwa kazi nzuri zinazofanywa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma ambaye ni kiongozi wa Baraza la Madiwani na maamuzi mazuri yanayofanywa na Baraza la Madiwani kwa maendeleo ya Dodoma” alisema Mwangosi.
Diwani wa Kata ya Madukani, Prof. Davis Mwamfupe alisema kuwa hospitali hiyo ipo katika kata yake. “Sisi ndio tunaona maendeleo haya na uboreshaji wa huduma za afya unaofanyika. Tuna kila sababu ya kumshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha afya za wananchi wake. Tuushukuru uongozi wa hospitali kwa kutupokea katika kutimiza dhamira yetu leo” alisema Prof. Mwamfupe.
Nae Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Kata ya Madukani, Jamila Ashery alisema kuwa hospitali hiyo ina mabadiliko makubwa ya kimiundombinu na huduma. “Hospitali ya ‘General’ haikuwa hivi, ila kwa utekelezaji wa Ilani ya CCM, hospitali imekuwa bora na ya rufaa na kufanya tunajivunia wana madukani” alisema Ashery.
Kwa upande wake Muuguzi Msaidizi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Najat Kayaga alisema kuwa wagonjwa wanaohudumiwa katika hospitali hiyo wanachangamoto nyingi na ujio wa viongozi hao wa CCM Kata ya Madukani umekuwa msaada mkubwa. “Siyo kila mgonjwa anayekuja ana uwezo. Hivyo, tunawaomba mzidi kutuona na wagonjwa wetu. Mtusaidie chochote kinachopatikana tukitumie kwa pamoja. Tuwasaidie ndugu zetu ili kujenga nguvu ya taifa” alisema Kayaga.
Mheshimiwa wa Kata ya Madukani Prof. Davis Mwamfupe akikabidhi baadhi ya misaada kwa mmoja wa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma wakati wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Kata ya Madukani (CCM) walipotembelea hospitali hiyo na kutoa misaada mbalimbali.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.