HOSPITALI ya Benjamin Mkapa (BMH) tarehe 13 Oktoba, 2020 imetimiza miaka mitano tangu ilipoanza kutoa huduma za afya kwa wananchi hapa Jijini Dodoma na mikoa ya jirani.
Katika kuadhimisha miaka hiyo mitano ya huduma, Hospitali iliandaa na kutoa bure huduma mbalimbali kuanzia tarehe 12 hadi 17, Oktoba, 2020 ambapo kulitolewa huduma ya upimaji afya kwa magonjwa ya Saratani ya matiti na shingo ya kizazi, Sikio, pua na koo, kisukari, moyo na mishipa ya damu na macho.
Aidha, huduma nyinginezo zilizotolewa ni elimu ya magonjwa ya figo na uchangiaji wa damu. Huduma hizi zilizohusisha uchunguzi wa afya zilitolewa kwa wananchi wa Dodoma na mikoa ya jirani.
Ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa Dkt. Alphonce Chandika aliwalisha keki baadhi ya wateja waliofika siku ya kwanza ya wiki la maadhimisho pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa BMH.
Akiongea kuhusu mafanikio ya Hospitali hiyo Dkt. Chandika alisema "Mwaka 2018 kwa kushirikiana na wadau kutoka Japan pamoja na Chuo Kikuu cha Dodoma, tulianza kupandikiza figo, mpaka sasa tumepandikiza figo kwa wagonjwa 13, wagonjwa wawili kati yao walipandikizwa figo na madaktari wazawa. Haya ni mafanikio makubwa ndani ya miaka mitano.
BMH ina mitambo ya uchunguzi wa maradhi kama ya MRI, CT-Scan, Fluoroscopy, Mammography, huduma za mionzi (X-ray), Endoscope na vifaa vingine vingi vya kisasa. Pia imekuwa ikitoa huduma za kawaida na za kibingwa kama vile magonjwa ya ndani (internal medicine), watoto (pediatrics), upasuaji, afya ya uzazi na kizazi, upasuaji wa njia ya mkojo, upasuaji wa koo, pua na masikio na kadharika
"Hospitali hii imekuwa ikifanya vizuri pia katika matibabu ya Kifua Kikuu na tumeweza kuanzisha huduma ya kutibu saratani kwa kutumia dawa, mipango iliyopo ni kuanzisha tiba kwa kutumia mionzi" alisema Dkt. Chandika.
Ikumbukwe Hospitali ya Benjamin Mkapa imeshafanya huduma za kibingwa kupitia Huduma Tembezi "Outreach" katika mikoa ya Iringa, Singida, Manyara na kadharika ambapo walipokuwa Iringa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, madaktari hao walilazimika kuongeza siku (zaidi ya siku 5 walizopanga) za kutoa huduma kutokana na maombi ya wagonjwa.
Vile vile, Dkt. Chandika alisema kuwa hospitali hiyo ilipozinduliwa mwaka 2015 ilikuwa na watumishi 22 wakuazimwa, lakini sasa kuna watumishi 453 baada ya Serikali kutoa kibali cha kuajiri na kuhamishia watumishi kutoka sehemu nyingine, alifafanua Mkurugenzi Dkt. Chandika.
Tazama picha za baadhi ya mitambo ya uchunguzi wa magonjwa.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.