Na. Dennis Gondwe, Majengo- DODOMA
WAFANYABIASHARA wa Soko kuu la Majengo katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wametakiwa kushirikiana kufanya usafi wa mazingira ili kuweka safi mazingira yao na kuepukana na magonjwa ya mlipuko.
Rai hiyo ilitolewa na mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Odilia Kotta alipoongoza mamia ya wafanyabiashara na wakazi wa Kata ya Majengo kuadhimisha miaka 59 ya Muungano kwa kufanya usafi katika Soko kuu la Majengo jijini hapa.
Kotta alisema kuwa dhamira ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ni kuhakikisha usafi wa mazingira ni kipaumbele katika kata zote. “Wito wangu, sisi wafanyabiashara na wananchi wa Kata ya Majengo ni sehemu ya wakazi wa Jiji la Dodoma. Lazima tuhakikishe kuwa agenda ya usafi ni sehemu ya utaratibu wetu. Tushirikiane pamoja kuliweka soko letu safi ili kuboresha mazingira, hali ya hewa na kuepuka magonjwa ya mlipuko” alisema Kotta.
Kotta ambae pia ni Afisa Mtendaji wa Kata ya Majengo alifurahia muitikio wa wananchi katika zoezi hilo la usafi. “Tupo hapa leo tarehe 26 Aprili, 2023 kwa ajili ya kuadhimisha miaka 59 ya Muungano kwa kufanya usafi wa mazingira katika Soko kuu la Majengo. Watu wamejitokeza wengi kufanya usafi na wamejituma kwa moyo na tumefanya usafi wa mazingira yote ya soko” alisema Kotta.
Kwa upande mwananchi aliyeshiriki kufanya usafi katika maadhimisho hayo, Subira Matonya alisema kuwa suala la usafi wa mazingira linatakiwa kuwa tabia ya wananchi wote. Alisema kuwa Muungano ni miongoni mwa tunu za Taifa, uendelee kulindwa na kudumishwa.
Halmashauri ya Jiji Dodoma imeadhimisha maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar chini ya kaulimbiu isemayo “Miaka 59 ya Muungano: Umoja na Mshikamano ndiyo nguzo ya kukuza uchumi wetu” kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.