SERIKALI mkoani Dodoma imepiga marufuku watu kuingiza mifugo kwenye chanzo cha maji Bonde la Mzakwe na atakayebainika kuingiza mifugo hiyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge wakati wa uzinduzi wa kampeni maalumu ya usafi wa mazingira, ambapo alisema anazo taarifa kuwa wako wananchi ambao wameanza kuingiza mifugo kwenye bonde hilo.
Aliwataka wafugaji wote pamoja na wananchi kuwa eneo hilo ambalo limetengwa kwa mipaka ni la bonde la maji la Mzakwe na kuongeza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kukilinda chanzo hicho muhimu.
“Ni marufuku kwa watu kuingiza mifugo kwenye chanzo cha maji bonde la Mzakwe na kwa yeyote atakayebainika kuingiza mifugo hatua zitachukuliwa dhidi yake,” alisema.
Bonde la Mzakwe ndio chanzo kikuu cha maji yanayotumika katika jiji la Dodoma na viunga vyake.
Hata hivyo, akizindua kampeni hiyo ya usafi, Mkuu huyo wa Mkoa alifurahishwa pia na Halmashauri ya Jiji kutokana na kusimamia vyema suala zima la usafi katika masoko. Pia kwa kuhamasisha uwekaji wa bidhaa kwenye meza maalumu kwa kuzingatia maelekezo ya kiafya.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Ofisa Masoko wa Jiji la Dodoma, James Yuna alisema mafanikio hayo yanatokana na kuendelea kuweka jitihada kubwa za usafi katika masoko yote.
Aidha mafanikio hayo pia yamechangia kuwafanya wafanyabiashara kukidhi maelekezo ya kiafya na kuepukana na magonjwa ya mlipuko yanayosababishwa na uchafuzi wa mazingira.
Ofisa huyo alisema Halmashauri ya Jiji itaendelea kuunga mkono juhudi za mkuu huyo wa mkoa za kufanya usafi mita tano kwenye maeneo ya makazi na biashara ili kuendelea kuweka mazingira mazuri.
Aidha alisema Jiji litaendelea kutoa mwito kwa wafanyabiashara wadogo maarufu machinga kufanya biashara zao kwa kuzingatia maagizo na maelekezo ya halmashauri.
Alisema maeneo hayo ni pamoja na kandokando ya barabara ili kuepusha ajali na usumbufu kwa waenda kwa miguu, kwa kuwa itatoa uhuru mkubwa kwa makundi ya watu kutumia barabara zilizopo ndani ya jiji ambao wamekuwa wakiweka pembezoni na kuathiri matumizi husika.
Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Takangumu jijini Dodoma Dickson Kimaro, alisema kuwa kwa sasa Jiji la Dodoma wamekuwa wakipokea tani 150 mpaka 180 za taka kila siku kwenye dampo la Chidaya, jiji likishirikiana na wadau kufanikisha usafi wa mazingira.
Chanzo: Tovuti ya Habarileo (www.habarileo.co.tz)
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.