Vikundi mbalimbali vya kijamii vikiwemo vya akina Mama na Vijana vimetoa shukrani zao za dhati kwa Mfuko wa Dunia wa Hifadhi ya Wanyama pori Tanzania (WWF) pamoja na Vodacom Foundation kwa mafunzo waliyowahi kuyatoa kwa vikundi hivyo, juu ya utengenezaji wa mifuko mbadala, kwani yamezaa matunda na kuwawezesha kujiajiri, kujitegemea na kujiongezea kipato.
Hayo yamesemwa na viongozi wa vikundi hivyo katika maeneo tofauti, walipotembelewa na walezi wa vikundi hivyo kutoka Halmashauri ya Jiji la Dodoma pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais, waliokuwa na jukumu la kufuatilia kwa karibu vikundi hivyo ili kujua maendeleo yao.
Mwenyekiti wa kikundi cha Walengwa, ambacho kinaundwa na wanafunzi kutoka Chuo cha Serikari za Mitaa Hombolo, Baraka Peter amesema kuwa kutokana na mafunzo hayo wameweza kutengeneza na kuzalisha idadi kubwa ya mifuko ya karatasi na kuiuza, hivyo wamekua wakipata faida kubwa ambayo imewawezesha wao kama wanafunzi kujilipia ada ya Chuo na mahitaji mengine ya kiuchumi tofauti na hapo awali ambapo walikua wakiwategemea wazazi pekee.
“Miongoni mwa manufaa tuliyoyapata kutokana na mafunzo yaliyofadhiliwa na WWF pamoja na Vodacom Foundation ni pamoja na kujikwamua kiuchumi, kwasababu tukishauza mifuko hii faida tunayopata tunagawana, kingine tumekua tukipata watu ambao wamekua wakihitaji kujifunza juu ya utengenezaji wa mifuko hii kutoka kwetu hivyo tumekua tukiwafundisha na wamekua mabalozi wazuri kitu ambacho kwa upande wetu imekua ni faida mojawapo pia” – alisema Baraka Peter.
Kwa upande wake Husein Hamis ambae ni kiongozi wa Kikundi cha Kishoka kilichopo Mtaa wa Chang’ombe Jijini Dodoma amesema kuwa mwanzoni walikua wakitengeneza mifuko mbadala na ilikua ikiwaingizia kipato lakini baada ya kuona kuwa kumekua na changamoto ya mifuko hiyo kuchanika na kutoosheka baada ya kuchafuka kwa kubebea vitu kama nyama na kadharika waliamua kujiongeza na kuanza kutengeneza vikapu ambavyo ndivyo vimekua vikihitajika sana kutokana na ukubwa na uwezo wa kubebea vitu tofauti kwa wakati mmoja kwa kuwa havichaniki kiurahisi, lakini pia vimekua vikiosheka na unaweza kuvitumia zaidi ya miaka mitano bila kuchaa.
Husein aliongeza kuwa licha ya uimara wa vikapu hivyo, pia vimewaongezea kipato kwani vinauzwa kwa bei nzuri zaidi ukilinganisha na mifuko mbadala ambapo vimekua vikiuzwa kwa shilingi elfu tatu, na mtu mmoja anauwezo wa kutengeneza vikapu kumi kwa siku, hali inayopelekea kuingiza Shilingi laki tisa ndani ya Mwezi mmoja kwa kila mwanakikundi.
“Tunawashukuru sana WWF, Vodacom Foundation, Halmashauri ya Jiji letu la Dodoma pamoja na Ofisi ya Mkamu wa Rais kwa mafunzo mazuri kwani kwa upande wangu, miongoni mwa faida ninayoipata kutokana na utengenezaji wa vifungashio mbadala ni kusomesha, nina mtoto anaesoma Kidato cha Sita hivyo nimekua na uwezo wa kumlipia ada pamoja na mahitaji mengine ya shule na familia yangu kiujumla” Alisema Husein Khamis.
Nae kiongozi wa kikundi cha Faraja ambacho kinaundwa na wanawake, Bi. Asha Bahoza amesema wao ni wanufaika wakubwa wa mafunzo hayo ambapo katika hali ya tofauti wanatengeneza mifuko ya Karatasi ambayo haipitishi maji.
Asha anasema baada ya kupata malalamiko ya vifungashio vya karatasi kuchanika baada ya kuloa au kubebea mizigo mizito waliamua kutafuta njia mbadala na kupata karatasi ambazo hazipitishi maji hivyo kutatua tatizo hilo na ubora wa bidhaa zao kupanda.
Akizungumzia mafaniko waliyoyapata wao kama kikundi alisema kwanza wamekuwa wakiaminika na kupata wateja wengi kutokana na ubora wa mifuko mbadala wanayoitengeneza, lakini pia wameondoa dhana ya kuwa tegemezi katika familia zao na jamii kwa ujumla kwani wamekuwa wakiendesha maisha yao na wengine kusomesha hali ambayo hawakuwa nayo hapo awali.
Changamoto kubwa iliyoelezwa na vikundi vingi isipokua kikundi cha Kishoka ni upatikanaji wa malighafi za kutengenezea mifuko hiyo mfano gundi ambayo walielekezwa kuitumia katika mafunzo kutopatikana kirahisi na kuwalazimu kutumia gundi ya maji ambayo imekua na ufanisi mdogo.
Aidha wamewaomba wafadhili ambao ni WWF na Vodacom Foundation kuongeza mafunzo zaidi ya utengenezaji wa bidhaa nyingine lakini pia kuwapatia mitaji ya kuanzia mara baada ya kumaliza mafunzo ili iwe rahisi kwao kupata bidhaa na kuyafanyia kazi yale wanayoyapata kwenye mafunzo.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Walengwa Baraka Peter (kulia) akiwa pamoja na wanakikundi wenzake kiwandani kwao.
Wanakikundi wakiwa wakionesha jinsi ya kutengeza mifuko mbadala mbele mwakilishi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Mwenyekiti wa Kikundi cha Kishoka Hussein Hamis akitengeneza kikapu.
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.