WITO umetolewa kwa kila Wilaya za Mkoa wa Dodoma kuhakikisha mifuko ya Elimu iliyoanzishwa na Halmashauri kwa lengo la kusaidia wanafunzi wenye uhitaji inafanya kazi kwa vitendo ili kuleta tija kwa wanafunzi wanufaika na jamii kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule alipokua Mgeni rasmi kwenye Hafla ya kuwapongeza walimu na wanafunzi waliofanya vizuri kwenye mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi katika shule ya Msingi Bahi Misheni iliyopo kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Bahi.
"Nitoe agizo kwa kila Wilaya zihakikishe Mifuko ya Elimu inafanya kazi kwa vitendo kama inavyofanya Bahi. Bahi mumeweka Elimu kwenye vitendo. Miaka 10 ijayo, Bahi itakua na wasomi wengi na maendeleo makubwa. Hii inadhihirisha mumemtafsiri Rais kwa vitendo" Amesema Mhe. Senyamule.
Kadhalika, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Gifty Msuya amesema kuwa wanatarajia kuutangaza mfuko wa Elimu Bahi ufike mbali zaidi na sio kuishia Bahi tu Bali hata nje ya nchi. Pia ameongeza kuwa Wilaya yake inakwenda kuvunja rekodi na kuiheshimisha Dodoma kitaaluma.
Hata hivyo, Mkurungenzi wa Halmashauri hiyo Bi. Zainab Mlawa, amesema Halmashauri yake imeshika nafasi ya 3 kwenye matokeo ya darasa la 7 mwaka jana (2023) na hafla hii ni utaratibu wa kila mwaka kutoa tuzo kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri ili kutoa hamasa zaidi na shule ya Bahi Misheni ndio ilikua ya kwanza kiwilaya.
Naye Mbunge wa Bahi Mhe. Kenneth Nollo, ametoa nasaha zake kwa kuitaka jamii kushirikiana kwa karibu kwenye suala la Elimu kwani Elimu ni ya jamii yote. Amesema ni lazima kuwe na jamii iliyoelimika, yenye maendeleo na inayoendelea kujifunza kila uchao na jambo hili liwekwe katika Mkakati.
Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ina jumla ya Shule za Msingi 86 zenye jumla ya wanafunzi 58,737 (Wav. 28,327 na Was. 30,410).
1 CDA Street, 40477
Anuani ya posta: 1249, DODOMA, TANZANIA
Simu: +255 26 232 4817
Simu ya kiganjani:
Baruapepe: cd@dodomacc.go.tz
Copyright ©2017 The City Council of Dodoma. All rights reserved.